Umaskini, ukosefu ajira changamoto kuu utekelezaji dira ya 2025

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:11 PM Aug 03 2024

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais, Mipango na uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo.
Picha:Mpigapicha Wetu
WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais, Mipango na uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo.

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais, Mipango na uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema umaskini pamoja na ukosefu wa ajira kwa Vijana wengi wa Kitanzania ni changamoto kuu zilizoshindwa kutatuliwa kikamilifu kwenye Dira ya maendeleo ya Taifa inayomalizika mwaka 2025/2026.

Prof. Mkumbo amezungumza hayo leo Jijini Mbeya wakati wa Kongamano la Kikanda, Kanda ya Kusini ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukusanya maoni ya wananchi katika uandishi wa dira ya maendeleo ya mwaka 2050.

"Mafanikio ni mengi yaliyotokana na dira ya Taifa ya 2025 lakini changamoto zipo zipo kwani ukuaji wa uchumi haukukua kwa kiwango ambacho kingefanikisha kuondoa umaskini, umaskini bado tunao lakini umepungua," amesema Prof. Kitila.

Amesisitiza wananchi wa mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe na Njombe kutoa maoni yao kikamilifu hasa kwa kuzingatia changamoto hizo za umaskini na ukosefu wa ajira ili kusaidia kupata dira itakayokuwa na suluhu ya changamoto za kiuchumi zenye kuondoa umaskini na kuzalisha ajira nyingi zaidi kwa vijana.

1

Aidha, ameeleza kuwa huma za kijamii nchini ikiwemo afya, elimu, maji na umeme ni miongoni mwa zilizoimarika zaidi na kukua kwa kasi kufuatia utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 inayoishia 2026.

Ametaja huduma hizo kuwa ni pamoja na huduma ya maji ambako 2000, mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa dira ya mwaka 2025 huduma hiyo ilipatikana kwa asilimia 32 pekee kwenye maeneo ya vijijini na kufikia 2022, imeongezeka hadi 77.

Pia amesema kaya asilimia 10 tu ndizo zilizokuwa zinapata huduma ya umeme na kufikia mwaka 2022 serikali imefanikiwa kufikisha huduma hiyo kwa asilimia 77.

Katika elimu Prof. Mkumbo amesema 2000 kati ya watoto 100 waliokuwa wanamaliza elimu ya msingi ni asilimia 10 pekee waliokuwa wanapata fursa ya kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na sababu mbalimbali ambako kwasasa kiwango kimeongezeka na kufikia 70 huku lengo likiwa ni kufikia  asilimia 90 mwaka 2025.