Temeke yaanza usafishaji damu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:04 AM Jun 15 2024
Mashine za usafishaji damu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mashine za usafishaji damu.

Hospitali ya Rufani ya Mkoa Temeke (TRRH) imeanza rasmi kutoa huduma za usafishaji damu (dialysis) ikiwa ni mara ya kwanza katika kuwahudumia wagonjwa wenye changamoto hiyo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali, Dk. Joseph Kimaro, alithibitisha kuwa huduma hiyo ilianza jana huku akisema hiyo ilikuwa siku muhimu kwa hospitali kwa kuwa huduma hiyo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu. 

Alisema hospitali imepata mashine 10 za usafishaji damu zilizonunuliwa kwa kutumia mapato ya ndani. 

Dk. Kimaro alisema huduma hiyo itasaidia wagonjwa wenye matatizo ya figo wanaoishi Temeke na maeneo jirani kama vile Kigamboni, Mkuranga na Pwani ambako hakuna hospitali inayotoa huduma kama hiyo.

Kwa mujibu wa  Dk. Kimaro, utekelezaji wa huduma hii si tu hitaji la hospitali hiyo  bali ni mpango wa serikali  unaolenga kufikisha huduma za kibingwa na bingwa bobezi kwa wananchi. Huduma hiyo mpya, alisema  itapunguza foleni na changamoto za umbali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Dk. Kimaro aliishukuru Mamlaka ya Usimamizi wa bandari Tanzania (TPA) kwa kuwezesha ukarabati wa jengo la kutolea huduma hiyo na kununua televisheni zitakazosaidia wakati wa kutoa huduma. 

Pia aliwataka wananchi kuendelea kufanya mazoezi na kufuata ushauri wa madaktari ili kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kuwa dawa zisipotumika kwa usahihi zinaweza kusababisha magonjwa kama ya figo.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Dk. Farida Ntonga, alishukuru uwapo wa mashine hizo na kusema timu ya madaktari na wauguzi wamepokea mafunzo ya kutosha, hivyo wananchi wawe na imani na wataalamu hao. 

Alisema mwaka jana hospitali ilipokea wagonjwa takribani 200 ambao walihitaji rufani kwenda Muhimbili lakini sasa kutokana na huduma hiyo mpya, rufani hizo zitapungua na wagonjwa watapata huduma katika hospitali hiyo ya mkoa.

Humphrey Tarimo, baba mkubwa wa mgonjwa wa kwanza kuhudumiwa na mashine hiyo, alielezea furaha yake kwa huduma hiyo kusogezwa karibu na makazi yao. 

Alisema walikuwa wakipata changamoto za usafiri kutokana na umbali wa hospitali, hivyo anaupongeza uongozi wa hospitali kwa ukarimu na utashi wao wa kujali wagonjwa.