TBS kuingia mtaani kusaka viwanda feki vya chuma

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 09:44 AM Jun 12 2024
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Athuman Ngenya
Picha: Maktaba
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Athuman Ngenya

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limepanga kuendesha msako kwa wazalishaji wa chuma ili kuwafungia wanaotengeneza bidhaa zisizokidhi viwango.

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Athuman Ngenya, alisema wakati wa mkutano kati ya TBS na wadau, Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Alisema watakagua kama wanaendelea kuzalisha bidhaa zisizokidhi viwango na watawachukulia hatua ikiwamo kuvifungia viwanda visivyofuata utaratibu.

Aidha, moja ya matakwa muhimu ya viwango vya bidhaa za chuma zinazozalishwa au kuingizwa nchini ni pamoja na kuandikwa taarifa zinazoonesha jina la mzalishaji pamoja na ukubwa wa bidhaa.

"Taarifa hizo ni muhimu kwa wanunuzi na watumiaji wa bidhaa kwani huwezesha kutoa mrejesho kwa mzalishaji husika pamoja na kufanya ufuatiliaji endapo itabainika kuwa na kasoro yoyote," alisema. 

Alisema taarifa muhimu kwenye bidhaa huziwezesha taasisi za udhibiti kuzitambua, kuzifanyia ufuatiliaji katika soko na kuchukua hatua stahiki kwa mzalishaji atakayebainika kukiuka matakwa ya sheria, kanuni na viwango.

Alisema pamoja na jitihada zilizofanywa na TBS ili kuhakikisha bidhaa hizo zinaandikwa taarifa muhimu ikiwa ni pamoja kutoa muda maalum ili kuhakikisha wanatekeleza takwa hilo muhimu, bado kuna baadhi ya wazalishaji ambao hawajatekeleza.

Alisema wazalishaji hao wamesababisha changamoto katika udhibiti na TBS itachukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa yeyote atakayezalisha bidhaa kinyume na matakwa ya viwango.

Mmoja wa wazalishaji, Ibrahimu Haji, alisema wataendelea kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango ili kuendana na ushindani wa biashara nchini.

Alisema kupitia kikao hicho, watayachukua maelekezo yote ambayo wamepewa na wataalamu kutoka TBS na kuyafanyia kazi ili kuendelea kuzalisha bidhaa bora na zenye viwango.