Taulo za kike kuchochea mahudhurio Mwanza

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 10:05 PM Mar 30 2024
Mwanahabari Grace Mbise akiwa na wanafunzi wa shule ya Sekondari Kayenze baada ya kuwakabidhi msaada wa taulo za kike.
Picha: Neema Emmanuel.
Mwanahabari Grace Mbise akiwa na wanafunzi wa shule ya Sekondari Kayenze baada ya kuwakabidhi msaada wa taulo za kike.

ZAIDI ya wanafunzi 400 wa kike kutoka shule ya sekondari Kayenze wilayani Ilemela, mkoani Mwanza, wamepewa msaada wa taulo za kike ili kuwanusuru na utoro ambao umetajwa kuwa chanzo cha kutokuzingatiwa masomo na kukatisha ndoto zao.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo  uliotolewa na mwanahabari Grace Mbise ikiwa ni siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Deogratus Paulo anaeleza kuwa ukosefu wa taulo za kike ni kikwazo kwa watoto hao huku ukichangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kujiingiza kwenye mambo ya siyofaa ili kupata bidhaa hiyo.

Kwa mujibu wa mwalimu huyo, uelewa mdogo wa wazazi na walezi kuhusu matumizi ya pedi kwa watoto wao na uwezo mdogo, husababisha watumie nyenzo nyingine kama vitambaa.

"Watoto wengi wa kike hapa unakuta wamepanga wanaishi peke yao hivyo unakuta pesa ya kununua taulo hawana, wanafunzi wengi wanashawishika na zawadi ndogondogo hasa zinazotoka kwa wavuvi, wengine hupata mimba na baada ya hapo hutoweka hata ukimtafuta kumpata ni tatizo," anaeleza.

Kwa upande wa Grace, anaeleza kuwa amesherekea siku yake ya kuzaliwa kwa kutoa msaada huo ili kuhamasisha wanafunzi kusoma na kuepuka vishawishi  kwa kisingizio cha kukosa huduma hiyo .

Kurwa Kadogosa ni mmoja wa wanafunzi walionufaika na msaada huo anaeleza kuwa wanapitia matatizo mengi pindi wanapokosa bidhaa hiyo, hivyo wanawaomba wadau wengine kujitokeza kwa wingi kuwasaidia ili waweza kuendelea na masomo  na kufikia malengo  waliyojiwekea.