TANI 12 za taka hutupwa katika ufukwe wa Rainbow kila mwaka sawa na tani moja kila mwezi, uchunguzi wa Nipashe umebaini.
Ufukwe huko ulioko Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam una taka za aina mbalimbali, zikiwamo za plastiki, mabaki ya vyakula, chupa za vioo na vifaa vya kielektroniki vilivyotupwa kiholela.
Katika uchunguzi wake, mwandishi wa Nipashe amebaini taka hizo zinatoka kwenye mito ambayo ni Mpiji Magohe, Mbezi, Feza, Mlalakua, Tegeta, Ng’ombe, Kigogo na Nyakasangwe, yote hutiririsha maji yake katika Bahari ya Hindi.
Imebainika kuwa kipindi cha msimu wa mvua wananchi hutupa taka zao katika mito hiyo ambayo humwaga maji yake katika bahari hiyo na kusababisha uchafu katika fukwe zilizoko Manispaa ya Kinondoni, ukiwamo wa Rainbow.
Maeneo mengine ya fukwe katika Manispaa ya Kinondoni yanayokabiliwa na adha hiyo ni Coco Beach, Magha na Kawe. Yote yanakumbwa na uchafuzi huo, hata kuibua maswali kuhusu uwajibikaji wa mamlaka husika na utekelezaji Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 (kifungu cha 55).
Sheria katika kifungu tajwa inatoa miongozo ya usimamizi wa taka hatarishi ili kuepuka madhara kwa mazingira na afya ya binadamu, ikielekeza kila mtu au taasisi inayohusika na uzalishaji, matumizi au utunzaji taka hatarishi inapaswa kuwa na mpango wa usimamizi wa taka hizo, ikiwa ni pamoja na utunzaji, uhifadhi na usafirishaji kwa njia salama.
Inaelekezwa katika sheria hiyo kuwa taka hatarishi lazima zitunzwe katika maeneo maalum kisha zichakatwe au kuteketezwa kwa njia inayozingatia usalama wa mazingira.
Sheria pia inaelekeza utoaji elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya taka hatarishi na kuhakikisha viwanda na taasisi zinazohusika na taka hizo zinapata leseni na idhini kutoka kwa mamlaka husika ili kuzuia uchafuzi wa mazingira na hatari kwa viumbe hai kutokana na taka hatarishi zinazozalishwa.
Hata hivyo, takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya tani 30 za taka zilikusanywa kwenye fukwe za Kinondoni kati ya Januari na Desemba mwaka jana, ikiwa ni kiashiria cha kiwango kikubwa cha uchafuzi katika maeneo hayo.
Biashara za chakula, kama vile mama lishe, pia zimeathirika kutokana na hali ya uchafu ambayo imesababisha watu wengi waogope kula au kununua chakula kwenye maeneo hayo.
Mfanyabiashara wa chakula, Maimuna Ally, ambaye amekuwa anafanya shughuli zake katika ufukwe wa Rainbow kwa miaka saba sasa, anaeleza kuwa uchafuzi wa mazingira umeathiri biashara yake kwa kiasi kikubwa.
Anasema harufu mbaya ya taka zilizoko kwenye ufukwe huo, imesababisha wateja wake kumkimbia, wakilalamikia hewa chafu.
"Tulikuwa tunauza chakula sana, kwa siku nilikuwa ninauza kilo 10 za wali, lakini sasa hata kilo mbili zinashindikana kuisha, hali hii inaonesha jinsi uchafuzi wa mazingira unavyoathiri moja kwa moja kipato cha sisi wafanyabiashara wadogo.
"Wateja wengi wameacha kuja kula hapa kwa sababu ya harufu mbaya na mandhari chafu yanayosababishwa na taka zinazozagaa kila mahali. Hii imeathiri kwa kiasi kikubwa idadi ya watu wanaokuja kupumzika au kufurahia mazingira ya ufukwe," anaongeza.
Mfanyabiashara mwingine wa chakula, Hawa Abdallah, anasema hali hiyo imepunguza idadi ya watu wanaotembelea ufukwe kwa burudani.
Anasema wateja wanahofia mazingira yasiyo salama kutokana na harufu mbaya kwenye fukwe hiyo, akisema inaathiri biashara yake kwa kupungua idadi ya wateja wanaonunua chakula.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Rainbow, Mohamed Mzee, anaeleza kuwa uchafuzi wa fukwe umeathiri afya ya wakazi wa eneo hilo kutokana na kuwapo pia mabomba ya sindano yaliyotupwa kiholela, akiyataja yanahatarisha maisha ya watoto na wakazi wengine wanaokanyaga sindano hizo bila kujua.
Mzee pia analalamikia maji machafu yanayotiririka baharini kupitia mito yanabeba bakteria na kemikali zinazoweza kusababisha magonjwa ya ngozi, matumbo na mfumo wa upumuaji.
"Wananchi wanavuta hewa chafu kutokana na harufu mbaya ya taka zinazooza, wengine wanaugua mara kwa mara kwa sababu ya mazingira haya," anasema Mzee.
Anaongeza kuwa hali hiyo ni mbaya zaidi kwa watoto, ambao wanacheza kwenye ufukwe huo bila kujua hatari zinazowakabili.
Wavuvi wa eneo hilo wanasema kuwa wanashindwa kuvua samaki wa kutosha kwa sababu taka hizo kuharibu mazalia ya samaki.
"Zamani tulikuwa tukivua samaki wa kutosha kwa matumizi na kuuza, lakini sasa samaki wamepungua sana, masharti ya uvuvi pia yamekuwa magumu kwa sababu ya uchafuzi wa mazingira," anasema Hamisi Athumani, mvuvi wa eneo hilo.
Baadhi ya shughuli za kitalii na biashara ndogo pia zimeathirika, wamiliki wa boti za kitalii wakilalamika kuwa idadi ya watalii wanaotembelea ufukwe wa Rainbow imepungua kutokana na mazingira machafu na harufu mbaya inayotokana na taka zinazozagaa.
"Tulikuwa tukipata watalii zaidi ya 20 kwa siku wanaokuja kufurahia safari za boti, lakini sasa tunapokea watalii wachache sana. Ufukwe huu umekuwa na sifa mbaya ya uchafu, na hiyo imeathiri biashara zetu," alisema Mariam Juma, mmiliki wa boti ya kitalii.
Mmoja wa madaktari bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Maxigama Ndosi, anasema taka hatarishi kama vile za hospitalini, akitolea mfano mabomba ya sindano, zinaweza kusababisha maambukizi ya magonjwa hatarishi kwa binadamu na wanyama.
Miongoni mwa magonjwa hayo kwa mujibu wa bingwa huyo ni tetenasi na kansa inayosababishwa na athari za muda mrefu za taka hatarishi.
"Taka hizi zikiachwa bila kusimamiwa ipasavyo, si tu kwamba zinaathiri afya ya binadamu, bali pia zinaweza kusababisha madhara kwa mazingira," anasema Dk. Ndosi.
Anaeleza kuwa kuna mwongozo wa kimataifa wa usimamizi wa taka hatarishi unaopendekeza utumiaji vyombo maalum vya kuhifadhi sindano na vifaa vingine vya hospitalini, lakini utekelezaji wake nchini bado uko chini ya viwango vinavyohitajika.
"Serikali inapaswa kuweka sheria kali na kuhakikisha hospitali zote, zahanati na vituo vya afya vinazingatia utunzaji taka hatarishi, kwa kutumia vyombo maalum na kuhamasisha usimamizi salama," anashauri.
Anapendekeza kuanzishwa programu za elimu kwa watoa huduma za afya na wananchi ili kuelewa madhara ya taka hatarishi. Dk. Ndozi anaamini hatua hizo zitasaidia kuzuia maambukizi yanayotokana na taka za hospitalini, huku zikihifadhi mazingira.
Dk. Ndosi anasema kuna haja serikali kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha miundombinu ya kuteketeza taka hatarishi ili kudhibiti athari za mazingira na afya.
Profesa wa Shule ya Sayansi na Teknolojia ya Uvuvi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Philip Bwathondi anasema taka za plastiki zinazoingia baharini zinaathiri viumbe wa majini na binadamu.
Anasema kuwa plastiki hizo husababisha vidonda kwa samaki na zinapoingia kwenye mwili wa binadamu kupitia ulaji samaki, huathiri afya, ikiwa ni pamoja na kusababisha kansa.
Prof. Bwathondi anashauri serikali kuweka ulinzi wa fukwe na kuimarisha sheria za kupambana na uchafuzi wa baharini ili kuepuka madhara yanayosababishwa na taka hizo na kuweka doria kudhibiti watu wanaobeba na kutupa taka kwenye mito na fukwe usiku.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED