Samia: Tusiwadharau wapinzani, tusiwaogope

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 05:43 AM Jan 19 2025
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan.

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka wanachama wa CCM wasiwadharau wapinzani na kuonya makada ambao wameanza kampeni mapema kuwa taarifa zao na ushahidi wa picha anazo.

Akifungua jana Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa CCM jijini hapa, Rais Samia alisema mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu, hivyo wanawajibu wa kuwa wamoja zaidi ili kukamilisha maandalizi ya ushindi.

“Tuna wajibu wa kulinda uhuru wa nchi yetu, hadhi ya utu wetu na heshima ya wananchi wetu. Wajibu huu tutautekeleza kwa kushinda uchaguzi na kuendelea kutoa uongozi bora ndani ya nchi yetu. Si siri kwamba hatima ya maendeleo ya taifa hili na watu wake, iko mikononi mwetu wana CCM,” alisema.

Aliwataka kutekeleza dhima hiyo kwa bidii kubwa na bila kuchoka na wasiruhusu kunyemelewa na kiburi cha kubeza wapinzani wao lakini pia wasiingiwe na pepo la kuwaogopa.

Alisema wanapambana nao kulinda heshima waliyopewa na wananchi ya kuliongoza taifa.

KAMPENI ZA MAPEMA

Kuhusu kampeni za mapema, alikemea wanachama wale wanaojipanga kwenda kugombea waache kufanya hivyo, kwa kuwa tayari amepata malalamiko na ushahidi wa picha za watu wanaofanya hivyo.

“Kuna wanaofanya misafara kwenda majimboni, watu wanaoitisha mikutano mikuu ya majimbo kwa kisingizio cha ufugaji au mambo mengine, dhamira ikiwa ni kujitambulisha kwa wanachama.Tunaomba tutoe onyo mapema,”alisema.

Alitaka wateuliwe wagombea wanaokubalika na kutounda makundi kwenye uchaguzi.

“Tunasema makundi ndani ya chama wakati wa kuomba, kwa sababu ya demokrasia waombaji ni wengi, kutakuwa na makundi mbalimbali. Lakini tunapopata wagombea wa chama chetu, tutakaowasimamisha, tunaomba makundi yasiendelee,” alisema.

 Pamoja na hayo, aliwaasa viongozi na watendaji wa CCM kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

“Chama hiki tunajitahidi kukibadilisha na kukijenga kama nilivyosema, kimuundo na kiundeshaji, kwa sababu ni chama chenye historia kubwa na kinachotegemewa. Viongozi na watendaji tuache kufanya kazi kwa mazoea,”alisema.

Aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha au kurekebisha taarifa zao kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura na kuwataka wajumbe wa mkutano huo kusimamia kwa nguvu kubwa ili wananchi wajitokeze kujiandikisha.

Alisisitiza viongozi kwenda kuwasikiliza wananchi na kutatua shida zao kwa kuwa kazi hiyo bado haijafanyika kwa uadilifu.

“Hakuna mashaka kuhusu ukubwa wa Chama Cha Mapinduzi. Hiki ndicho chama kikubwa kuliko vyote hapa nchini. Sisi ni chama kikubwa kimuundo, kioganaizesheni, kihistoria na hata kwa idadi ya wanachama,”alisema.

Alieleza kuwa kupitia zoezi la usajili wa wanachama kidijitali, hadi kufikia Disemba 31, 2024 CCM ilisajili wanachama 12,104,823.

ACHENI MAZOEA

Rais Samia alisema CCM itaendelea kufanya mageuzi kimfumo, utendaji na uendeshaji hivyo wanachama na viongozi wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia uzalendo na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
 
 Alisema  chama kimeendesha mafunzo ya kiutendaji nje na ndani ya nchi ambapo kwa upande wa nje ya nchi mafunzo yalitolewa zaidi katika nchi za China na India.
 
 "Tumerahisisha shughuli za kiutendaji wa Chama na jumuiya zake kwa kununua vyombo vya usafiri kuanzia kwenye mashina hadi mikoa, magari 194 yamesambazwa katika ofisi 149 za wilaya, magari 33 ofisi za CCM mikoa yote, magari tisa ambapo matatu kila jumuiya za CCM,” alisema.

Rais Samia alitangaza neema kwa mabalozi wa CCM baada ya kutangaza kuwa Chama kipo katika mchakato wa kutafuta usafiri kwa mabalozi.
 
Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Emmanuel Nchimbi, alisema mkutano huo una ajenda nne za uchaguzi wa Makamu wa Mwenyekiti CCM Tanzania Bara, taarifa ya NEC ya utekelezaji wa kazi za chama, taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na marekebisho ya katiba ya CCM ya mwaka 1977.