Sakata la 'Binti wa Yombo' lafukuta

By Jenifer Gilla ,, Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:47 AM Aug 21 2024
Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi.
Picha: Mtandao
Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi.

CHAMA cha Mawakili Tanganyika (TLS) kimelitaka Jeshi la Polisi kumfikisha mahakamani mtu anayetajwa 'afande’, anayedaiwa kutuma vijana wanne kumbaka na kumlawiti binti anayedaiwa mkazi wa Yombo Dovya, wilayani Temeke, mkoani Dar es Salaam, kisha video ya ukatili huo kusambazwa mitandaoni.

Pia kimetoa wito kwa Jeshi la Polisi na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuimarisha madawati ya jinsia katika majeshi, ikiwamo kuweka watumishi wenye weledi wa kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia ipasavyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi alisema chama kinapongeza hatua za kufikishwa mahakamani wanaodaiwa kutenda uhalifu huo, lakini wanataka aliyesababisha kufanyika kitendo hicho afikishwe mahakamani mara moja.

Alisema chama hicho kimedhamiria kumweka wakili atakayefuatilia maendeleo ya shauri la kesi hiyo, ili kuhakikisha haki ya binti huyo inapatikana na waliohusika wanachukuliwa sheria.

Wakili Mwabukusi pia alipongeza hatua zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi kumwajibisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Theopista Mallya kutokana na kauli yake iliyotafsiriwa kama kupuuzia madhila makubwa aliyoyapata binti huyo.

"TLS itaona namna bora ya kuweka wakili atakayekuwa akifuatilia ili kuona maendeleo ya shauri lile, yatakavyokuwa yakiendelea na kuhakikisha kuwa haki za binti yule hazipotei," alisema Wakili Mwabukusi.

Alisema chama hicho kinatoa wito kwa Jeshi la Polisi na wizara yenye dhamana kuimarisha madawati ya jinsia kwa kuweka watu wenye uwezo na wanaochukizwa na vitendo hivyo ili kuyashughulikia kwa weledi.

Katika ukurasa wake wa X, Wakali Peter Madeleka, aliandika: "Leo (jana) tarehe 20 Agosti 2024, Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma imesajili malalamiko namba 000058901 ya Paul Emmanuel Kilasa Kisabo dhidi ya …(anataja jina anayedaiwa ofisa wa jeshi) anayedaiwa kutuma vijana wambake na kumlawiti binti wa Yombo."

Malalamiko hayo yanasema kuwa ‘afande’ (jina halipo) katika tarehe isiyojulikana Mei mwaka huu eneo la Swaswa, Jiji la Dodoma alitenda kosa la kuwezesha ubakaji kwa kundi (akataja majina ya washtakiwa wanne wanaodaiwa kubaka na kulawiti) dhidi ya binti huyo, jambo ambalo ni kinyume na utu. 

Mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alisema binti huyo kukaa mikononi mwa Jeshi la Polisi si salama na akapendekeza ahifadhiwe na taasisi za haki za binadamu.

"Inatakiwa taasisi za haki za binadamu zimchukue huyu binti kisheria kutoka polisi. Tanpol siyo mahala salama kwa binti huyu," alidai Zitto.

"Badala ya kupata msaada huko, atakuwa ameteseka sana kisaikolojia. THRD COALITION nini kinawashinda kumchukua binti chini ya uangalizi wenu? 

"Kumwacha huyu binti Polisi kwa siku moja zaidi ni kumtesa sana, hao Polisi wataanza kumshambulia kuwa amemfukuzisha mwenzao," alidai.

Kauli hiyo ya Zitto inafanana na ile iliyotolewa na Shirika la Msichana Initiative pamoja na mashirika yanayotetea haki za wanawake Dar es Salaam, ambao wametaka binti huyo apate msaada wa kuhifadhiwa na taasisi tofauti na Jeshi la Polisi ili haki ionekane inatendeka.

Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi, alisema ni vyema anayedaiwa kuagiza vijana waliotekeleza kitendo hicho akakamatwa.

"Aliyeagiza yale yote yafanyike, yuko wapi? Kwani sheria zetu ni za watu fulani na wengine haziwagusi? ‘End impunity’, afande akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria," alisema Rebeca.

WALIOPOTEA

Katika hatua nyingine, Wakili Mwabukusi amesema Baraza la Uongozi la TLS imeazimia kuwafungulia mashtaka kwa majina yao wale wote wanaotajwa kuhusika kwenye kadhia ya kukamata, kuteka na kutesa kiholela wananchi na imeandaa timu ya mawakili kwa ajili kufanya kazi hiyo.

Alilitaka Jeshi la Polisi kuwaeleza Watanzania kuwa uchunguzi wao kuhusu watu hao umefikia wapi na kuwa wanalifuatilia jambo hilo kwa karibu na hatua sizipochukuliwa hawatosita kufanya hivyo.

"Ni wito wetu kwa mamlaka, kutoa orodha ya wananchi wasiojulikana walipo, hawa ni Watanzania, uhai ni kitu cha thamani kuzidi kitu kingine chochote. Tunalitaka Jeshi la Polisi kutoka mbele za umma na kuwaeleza wamefikia wapi, uchunguzi kuhusu watu hao umefikia wapi," alisema.

Wakili Mwabukusi alisema TLS pia inatoa  wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kurejesha huduma za kijamii kwa wananchi wa Ngorongoro, ikiwa ni pamoja na kurejesha vituo vya kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura ili kuhakikisha wanaitumia haki yao ya kikatiba katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwezi Novemba mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Alisema kuwa kwa kutambua uzito wa suala hilo, Baraza la Uongozi la TLS limeunda kamati maalum ya kuchunguza na kufuatilia kwa karibu mgogoro wa Ngorongoro, ikijumuisha wanasheria wabobevu aliowataja kuwa ni Dk. Rugemeleza Nshala, Tike Mwambipile, Bumi Mwaisaka, Laetitia Ntagazwa na Paul Kisabo.

Kwa mujibu wa Rais huyo wa TLS, kamati hiyo imepewa jukumu kadhaa, ikiwamo kufanya mashauriano na taasisi mbalimbali pamoja na kutembelea maeneo yenye migogoro, ili kufahamu uhalisia wa hali hiyo, kupitia sera, sheria na mazoea yanayohusiana na umiliki wa ardhi kwa wazawa na kuhakikisha haki za msingi za raia zinazingatiwa kwa mujibu wa katiba, sera na sheria za nchi.

Kamati hiyo pia itaandaa kongamano la kitaifa kuangazia namna bora ya kusimamia maendeleo huku ikilinda haki za wazawa katika ardhi zao za asili na kuchunguza mashauri na hatua zilizochukuliwa kisheria ili kubaini kama kweli kuna watu waliokubali kuondoka kwa hiyari na wale waliokataa kuondoka kutoka kwenye ardhi yao ya asili.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pia kimeitaka serikali kusikiliza wananchi wa eneo hilo kwa lengo la kupata ufumbuzi wa kudumu na kuepuka maafa.

Pia kimeitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kurejesha majina ya wapigakura hao katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.