RIPOTI YA UCHUNGUZI -2: Mifugo, uchimbaji madini vyaweka rehani uhai wa Hifadhi ya Taifa Saadani

By Sanula Athanas , Nipashe
Published at 07:23 PM Nov 01 2024
Makazi katika  Hifadhi ya Taifa Saadani.
Picha: Maktaba
Makazi katika Hifadhi ya Taifa Saadani.

UHAI wa Mbuga ya Wanyama Saadani uko shakani. Kile ambacho sheria zinazuia ili kulinda uasili wa mbuga, ndicho kinafanyika. Zile kanuni zinazolenga kukinga hifadhi, ndizo zinavunjwa. Mikono ya waliotarajiwa kutetea na kulinda urithi wa nchi na dunia, inaonekana kufaganzi.

Haya yanatokea wakati wasimamizi wa mbuga wakijipanga kuifanya Saadani kuwa Kitovu cha Utalii wa Ndani; wakianzisha utalii wa wikiendi (Ijumaa hadi Jumapili) kwa wakazi wa Dar es Salaam kwa safari za treni maalumu huku wakipanga kuongeza safari za ndege na boti kwa watalii wanaopitia Zanzibar. 

Watalii wanaoingia au kutoka nchini, kwa kupitia Zanzibar na Dar es Salaam, huenda wakashindwa kuepuka kishawishi cha kuwa na mapumziko ya siku mbili au tatu katika hifadhi ya Saadani kabla ya kuanza au kuendelea na safari zao kwingine. 

Hayo yanaweza kutokea na kushamiri iwapo mbuga haitavurugwa kwa kuharibu ikolojia yake na kukatisha uhai wa mimea na wanyamapori ambavyo ni sehemu kubwa ya uasili na utajiri wake. 

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, anashauri katika ripoti zake za 2020/21 na 2021/22, "…serikali ichukue hatua stahiki kunusuru mfumo wa ikolojia wa Hifadhi ya Taifa Saadani." 

Kunusuru Saadani ni kuacha kutupa chochote mbugani ambacho hakikuwamo; kuondoa mifugo mbugani ili kuepusha mifugo kuambukizwa au kuambukiza magongwa kwa wanyamapori, kupunguza au kuondoa kabisa kelele za binadamu na shughuli hasi kwa uasilia wa hifadhi; na kutoongeza au kupunguza mimea – miti hata maua ndani ya hifadhi. 

Kifalsafa, hakuna uasili ulio nje ya utawala wa binadamu. Ataupenda uasili. Ataulea. Atautumia. Lakini atauharibu au kuuua. Hakuna mahali ambako binadamu hajaathiri – vizuri au vibaya – mipaka, maendeleo, uhai na uhalisia wa watu, vitu na uzuri wake.

Hata hivyo, hii si sababu ya kuharibu kila kitu hata chenye thamani na faida kwa watu na jamii. Hii ndio maana mbuga zinalindwa kisheria kwa manufaa ya jamii nzima ya dunia. 

Hapa ndipo inaingia Saadani na mbuga nyingine. Adui wa uhalisia aliyebakia na asiyetawalika haraka, ni “mabadiliko ya tabianchi.” Lakini naye, kwa sayansi iliyopo, aweza kutabiriwa, kuandaliwa mikakati na hatimaye kupunguza nguvu zake kwa uasili wa mtu na mazingira yake. 

Hili pekee ndilo linahalalisha kuwapo sheria na kanuni za kulinda uasili wa hifadhi na familia za viumbe waliomo. 

Kwa hiyo, kukata miti hifadhini, kujenga kiwanda hifadhini kwa ajili ya kuzalisha chumvi, kubakiza kijiji cha watu wapatao 1,500 ndani ya hifadhi, ambao wataongezeka na hatimaye kuhitaji shule, zahanati na huduma nyingine za msingi; ni kulea makusudi ya kuua mbuga na uasili wake.  

Kukata mikoko ambayo inabugia hewa-ukaa kwa wingi kuliko mimea mingine, kunaacha jamii bila ulinzi. Kupiga kelele maeneo mbalimbali mbugani kunafukuza wanyamapori na kupunguza au kuondoa kabisa thamani ya hifadhi. Sheria ya Hifadhi za Taifa ya Mwaka 1959 inazuia yote hayo. 

Ukiingiza mafuta na kemikali nyingine za mitambo, na vitu hivyo kumwagika au kumwagwa mbugani, mimea ambayo haihami, ama hukauka, huathirika vibaya au hufa, wataalamu wameonya. 

Mbuzi, mbwa na kuku wanaoranda misitu na mbuga ya Saadani, siyo wakazi halali na wa asili hifadhini. Hawa huweza kuangamizwa na wanyamapori, au hata kuchumbia wanyamapori kukaribia makazi ya binadamu na kuwadhuru au kuwaua.

Aidha, mifugo mbugani, kama ulivyo uchimbaji madini, kwa maoni ya CAG, ni shughuli ambazo “zinahatarisha mfumo wa ikolojia ndani ya hifadhi na hivyo kusababisha kutokuwapo uhakika wa uendelevu wa Hifadhi ya Taifa Saadani." 

Saadani ina mto maarufu – Wami, wenye ikolojia inayohifadhi miti ya mikoko ambayo ni maarufu pia kwa kuhifadhi uoto wa asili wa misitu ya pwani na nyika, samaki, mamba, viboko na ndege wa majini.

Saadani pia ina misitu minene ya ukanda wa pwani (Zaraninge); ina makundi ya tembo, nyati, pundamilia, swala na simba; ina utalii wa fukwe na utalii wa boti ili kuona mamba na viboko. 

Mradi wa uzalishaji chumvi uliomo ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani.
Hata hivyo, yanayotendeka ndani ya Saadani yanakinzana na sheria za hifadhi nchini, na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26), ambao pamoja mambo na mengine, unalenga kuimarisha vivutio vya utalii ili vichangie zaidi katika Pato la Taifa na kutoa fursa za ajira.

Kwa mujibu wa mpango huo, ifikapo mwaka 2026, idadi ya watalii nchini inatarajiwa kufikia milioni tano na mapato ya dola bilioni sita kwa mwaka, Hifadhi ya Taifa Saadani ikiwa sehemu ya mkakati huo wa kuwavutia wageni.

Mazingira ya sasa ya Saadani yanakinzana pia na Programu ya Utalii ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya 2020 – 2030 inayohimiza nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuhakikisha kunakuwa na utalii endelevu na kuondosha vikwazo vya utalii na uhifadhi katika ukanda huo. Tanzania ni mwanachama mwasisi wa SADC. 

Unahitaji kujua fikra na mipango ya sasa ya Saadani ili uelewe kuwa lolote la kukwaza hifadhi hiyo linaweza kuitwa hujuma ya makusudi. 

Unahitaji kujua, kwa mfano, kuna matangazo yanakuja kwa wanaotaka kufanya uwekezaji chanya – hoteli na kumbi za starehe na mengine kwa watalii, ili kuinua ubora na umaarufu wa hifadhi. 

Kwa mfano, aliyekuwa Mkuu wa Hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ephraim Mwangomo (sasa amehamishiwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere), anasema kuna mpango wa kujenga gati la muda ili mbuga iwe inafikika kwa watalii wanaokuja kwa boti kutoka Dar es Salaam na Zanzibar. 

Mwandishi ameoneshwa vifaa vya ujenzi. Kazi inapaswa kukamilika katika miezi mitatu ijayo; huku likisubiriwa gati la kudumu linalojengwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. 

Tayari amepatikana mwekezaji kwa ajili ya usafiri wa boti, Aljazeera Marine Tours and Safaris ambaye shughuli zake za usafirishaji watalii zilipangwa kuanza Julai mwaka huu – akibeba watalii kutoka Zanzibar. 

Utavutiwa na mpango kabambe wa kupeleka makundi ya watalii kwa ndege kutoka Zanzibar na Dar es Salaam hadi kiwanja cha ndege kilichomo ndani ya hifadhi “kwa bei chee” kama alivyoitaja Kamishna Mwangomo – dola za Marekani 1,200 kwa mtu mmoja au kundi la watalii watakaokuwa wanakwenda mbugani wakati huo. Anaitaja ni safari ya robo saa kutoka Zanzibar hadi hifadhini. 

Lakini zogo linalotishia hifadhi ya Saadani, halihusu mwekezaji na wakazi peke yake. Linahusu pia wanyama na wakazi wa mbugani kama ilivyo nchi nzima. 

Katika ripoti yake, CAG Kichere anasema kulikuwa na visa 42 vya migogoro kati ya binadamu na wanyamapori kwenye hifadhi za taifa nchini vilivyosababisha vifo vya watu 26 na wengine 77 kujeruhiwa kwa mwaka 2021/22. Mwaka 2020/2021, kulikuwa na visa 31 vilivyosababisha vifo vya watu 20 na majeruhi 66. 

CAG anataja sababu kuu ya vifo na majeruhi ni binadamu kuingilia hifadhi za wanyamapori, kama inavyoshuhudiwa Saadani kwa sasa. 

Festo Ndahani (50), mkazi wa kitongoji cha Makupani, ni shahidi wa zogo kati ya wanyamapori na binadamu. “Agosti 2021, nyati alinijeruhi kwenye mkono wa kulia na mguu wa kushoto,” anaonyesha.

"Kipindi hicho nilikuwa kibarua katika Kampuni ya Sea Salt Limited. Nyati alinikuta ninakata minyaa kwa ajili ya kupanda kwenye mabwawa ya chumvi. Kama si yowe niliyopiga wanakijiji wakaja kuniokoa, nisingekuwa hai,” anaeleza.

"Nilikaa Muhimbili (Hospitali ya Taifa) kwa wiki mbili. Matibabu yalikuwa Sh. 950,000. Wauguzi waliniambia 'nenda nyumbani, ukipata fedha, utalipa deni lako',” Ndahani anabainisha hajawahi kulipa. Hana kazi. 

Makazi yanayoondolewa hifadhini
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Makupani, Mzee John Mbota anasema changamoto kubwa zinazowakabili ni kuvamiwa na wanyamapori wakali, hasa chui na nyati. Analitaja tukio la Aprili 2022 la kuvamiwa na nyati lililosababisha kifo cha mwanakijiji.

 Kamishna Msaidizi Mwangomo alithibitisha kuwapo uvamizi wa chui katika makazi ya wananchi na kuchukua mbuzi, hasa katika kijiji cha Saadani. 

Mwandishi aliamua kuingia hifadhini kujionea mwenyewe hali ilivyo. Kwa saa tatu alisubiri gari aina ya Noah kutoka Bagamoyo, lipate abiria 12 ili kwenda kwenye mradi wa chumvi. Ni kilometa 44 hadi kijiji cha Gama kwa nauli ya Sh. 5,000. Baada ya hapo kuna safari ya kilometa 11 kwa pikipiki (bodaboda) kwa malipo ya Sh. 8,000 kukifikia kitongoji cha Makupani.

Hii ni safari inayomwanzishia msafiri utalii kwa kuona aina mbalimbali za wanyamapori hifadhini kama vile tembo, simba, nyati na nyani ambao ndiyo wengi zaidi hifadhini (2,170). Msafiri anatalii mwanzo hadi mwisho bila kulipa chochote kwa mamlaka ya hifadhi – SANAPA.

Hapa kuna vibanda vilivyojengwa kwa miti na kukandikwa kwa udongo, huku vikiezekwa kwa makuti na vichache kwa mabati. Pia kuna nyumba nne zilizojengwa kwa matofali ya saruji na kuezekwa kwa mabati; na vibanda vingine viwili vilivyojengwa kwa mabati kuanzia chini hadi paa. 

Pembeni kuna nyumba imara ambayo Mzee Mbota anasema ni kwa ajili ya viongozi wa kampuni hiyo; huku kuku wakiparua, mbwa wakirandaranda karibu na mitambo ya uzalishaji chumvi.

Yalipo mabwawa (vyungu) ya kuvunia chumvi, pembeni (karibu na barabara) kuna mabango makubwa yenye maneno tisa (9) yaliyoandikwa kwa herufi kubwa kwa lugha za Kiingereza (juu) na Kiswahili (chini), yanayosomeka: PRIVATE PROPERTY, PHOTOGRAPH PROHIBITED (MALI BINAFSI, MARUFUKU KUPIGA PICHA).

Ni katazo ambalo Kamishna Msaidizi Mwangomo alilalamika ni kinyume cha sera yao, kwamba picha ni sehemu ya utalii, picha ndiyo biashara ya utalii, ndiyo raha yenyewe ya utalii, hivyo mabango hayo yanasababisha mgongano wa chumvi na utalii.

 Alirejea historia, kwamba wakati SANAPA inaanzishwa mwaka 2005, vijiji vya Saadani na Buyuni havikuondolewa mbugani, lakini "baadaye ikabainika kitongoji cha Uvinje (kijijini Saadani) kinaingilia mno shughuli za hifadhi."

 Kwa mujibu wa Sensa ya Watu ya Mwaka 2012, kijiji cha Saadani kilikuwa na wakazi 1,433 wakati kijiji c ha Buyuni kilikuwa nao 206.

Kamishna Msaidizi Mwangomo alisema tayari wakazi wa kitongoji cha Uvinje wamefanyiwa taratibu za kulipwa fidia ili kupisha eneo la hifadhi, akifafanua, "…mwaka 2014, kaya 22 zililipwa fidia ya jumla ya Sh. 769,539,770 (milioni 769.54/-). Malipo ya ziada ya Sh. 287,631,000 kwa wananchi 42 yanaandaliwa."

Kuhusu hoja ya ekari 728.17 kuendelezwa na Kampuni ya Sea Salt Limited bila kibali cha TANAPA, Kamishna Mwangomo alisema utatuzi wake uko chini ya Kamati Teule ya Mawaziri Wanane iliyofika Saadani Oktoba 2019, kushughulikia mgogoro huo unaoendelea.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sea Salt Limited, Ajay Sengar, amemweleza mwandishi kuwa kuna mgogoro wa eneo kati yao na TANAPA; na kwamba wanasubiri utatuzi wake toka mamlaka za serikali.

Kwa mujibu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kampuni hiyo ilisajiliwa nchini mwaka 1998 ikiwa na mtaji wa Sh. bilioni 10 na shughuli zake kuu ni uchimbaji chumvi na madini mengine.

Kamishna wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Nathaniel Nhonge, amemwambia mwandishi kuwa mzozo huu “unashughulikiwa na Kamati ya Mawaziri Wanane” iliyoundwa na Rais John Magufuli mwaka 2019.

 Kamishna wa Madini, Dk. Abdulrahman Mwanga, alimthibitishia mwandishi kuwa leseni Na. ML 05/92 ilitolewa kwa Kampuni ya Sea Salt Limited kwa mujibu wa sheria kwa kuwa mwekezaji huyo alifuata taratibu za kupewa leseni ya uchimbaji madini.

Profesa wa Mifumo ya Ikolojia, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Idara ya Mifumo Ikolojia na Uhifadhi, Pantaleo Munishi amemwambia mwandishi kuwa takaoevu zitokanazo na uchimbaji madini ni hatari kwa afya ya viumbe hai na mazingira iwapo hazitadhibitiwa.

Prof. Munishi anafafanua, "Isivyo bahati taka kama hizi madhara yake huonekana baada ya muda mrefu. Mimi ninashauri uchimbaji madini kwenye maeneo ya hifadhi uachwe kwa sababu una athari kubwa katika mifumo ya kiikolojia kwa wanyama na mimea.”

Bakari Mtiri, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, Moshi, anashauri elimu itolewe kwa wananchi na wawekezaji ili kuwanusuru wanyamapori.

 Ofisa Miradi wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), Clay Mwaifwani, anashauri Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) litumie mamlaka yake chini ya kifungu cha 99(2) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004, kufika eneo la uzalishaji chumvi Saadani na kufuatilia ni kwa kiasi gani shughuli hizo zinaathiri mazingira na mfumo wa ikolojia wa hifadhi.

"Iwapo ufuatiliaji utaonesha mzalishaji chumvi alikiuka sheria kwa kutofuata masharti ya Tathmini ya Athari za Mazingira (EIA), NEMC watapaswa kutumia mamlaka waliyonayo chini ya kifungu cha 100(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 kumtaka mzalishaji kusafisha mazingira, pia kuchukua hatua zitakazoelekezwa ili kuyarudisha mazingira katika ubora wake wa awali,” anasema.

"NEMC wakitekeleza wajibu wao kikamilifu, watalinda hifadhi za taifa, wataongeza mapato ya serikali na zaidi ya yote, watawalinda wanyamapori na kuwahakikishia kuishi katika mazingira safi na salama," anashauri.

Kamishna Mwangomo alisema, SANAPA ambayo ni Hifadhi ya Taifa ya 13 kuanzishwa nchini kati ya 22 zilizopo chini ya TANAPA, sasa ina waajiriwa 83; kati yao, 18 ni wanawake; na asilimia 60 ya waajiriwa wote ni askari-pori.