RIPOTI MAALUM: Taka zatishia usalama, uchumi fukwe za Dar -2

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 08:31 AM Feb 19 2025
Taka ufukweni.
Picha: Grace Mwakalinga
Taka ufukweni.

KATIKA sehemu ya kwanza ya ripoti hii jana, tulieleza hali ya uchafuzi wa mazingira kwenye ufukwe wa Rainbow, tani 12 za taka hutupwa kila mwaka ufukweni huko, ikiwa ni wastani wa tani moja kila mwezi. Endelea...

Kimsingi kinachoshuhudiwa ufukweni Rainbow ni matokeo ya kushindwa kutekeleza Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004, hasa kifungu chake cha 55 kinachotoa miongozo ya usimamizi wa taka hatarishi ili kuepuka madhara kwa mazingira na afya ya binadamu.

Sheria hiyo inaelekeza kuwa kila mtu au taasisi inayohusika na uzalishaji, matumizi, au utunzaji taka hatarishi, inapaswa kuwa na mpango madhubuti wa usimamizi wa taka hizo, ikiwa ni pamoja na uhifadhi, usafirishaji na utunzaji taka hizo kwa njia salama.

Sheria pia inaelekeza utoaji elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya taka hatarishi na kuhakikisha viwanda na taasisi zinazohusika na taka hizo zinapata leseni na idhini kutoka kwa mamlaka husika. Lengo ni kuzuia uchafuzi wa mazingira na hatari kwa viumbe hai kutokana na taka hatarishi zinazozalishwa.

Mkaguzi wa Mazingira Manispaa ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, Alban Mugyabuso, anasema watu wengi hawajui madhara ya kutupa taka ovyo. 

Anasema taka hizo zinakusanyika kwenye fukwe, hasa kipindi cha mvua, na kuathiri mandhari ya fukwe na viumbe hai wa baharini.

Mghyabuso anasema Manispaa ya Kinondoni imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na tatizo hilo na inaendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa usafi na usimamizi wa taka.

Ofisa huyo anasema wametoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya kutupa taka kwenye mito na fukwe. Pia wanajenga miundombinu bora ya ukusanyaji taka katika maeneo yanayotiririsha maji kwenye mito na baharini.

"Changamoto kubwa inabaki kwenye kupata ushirikiano kutoka kwa jamii ili kuhakikisha kuwa sheria na miongozo ya usimamizi wa taka inazingatiwa kikamilifu," anasema.

Mugyabuso anaongeza: "Baadhi ya viwanda na taasisi hazifuatilii miongozo hii na wananchi wengi hawaelewi vizuri kuhusu usimamizi wa taka hatarishi, inahitaji ushirikiano mkubwa kati ya serikali, sekta binafsi na jamii kwa ujumla."

Anasema Manispaa ya Kinondoni imechukua hatua kadhaa dhidi ya zaidi ya watu 250 waliokamatwa kwa tuhuma za uchafuzi wa mazingira katika mwaka jana (2024). 

"Wengine wamepewa adhabu ya kulipa faini ya kuanzia Sh. 50,000 hadi Sh. 300,000 na wengine walielimishwa kuhusu madhara ya uchafuzi wa mazingira," anasema ofisa huyo.

Mugyabuso anasisitiza kuwa ni muhimu kuendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya taka hatarishi na umuhimu wa usimamizi wa taka. 

"Tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara katika viwanda na taasisi zinazohusika na taka hatarishi, tunatoa elimu kwa wananchi na tunahakikisha kuwa mifumo ya ukusanyaji taka katika maeneo ya umma inaboreshwa," anasema.

Mugyabuso anasema Manispaa ya Kinondoni imeweka vidakia taka katika maeneo kadhaa, ukiwamo Mto Feza ambako taka zinazokwama kwenye vidakia hivyo, husafirishwa na kuchakatwa. 

"Mpango wetu ni kuweka vizuia taka katika mito yote minane inayomwaga maji yake baharini ili kuzuia uchafuzi wa fukwe," Mugyabuso anasema na kuitaja ni  hatua muhimu katika kupambana na uchafuzi wa mazingira, akisisitiza vidakia taka vitasaidia kuzuia taka zisifikie maeneo ya fukwe.

Mhandisi wa Mazingira kutoka Baraza la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Boniface Kyaruzi, anasema uchafuzi wa taka za plastiki na hospitalini unahatarisha mazingira ya baharini na viumbehai. 

Kyaruzi anasisitiza kuwa ni muhimu kuwapo ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi katika kutekeleza sheria za mazingira, ikiwa ni pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maji ya Mwaka 2009, ambazo zinaelekeza udhibiti wa uchafuzi wa fukwe na vyanzo vya maji.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Human Dignity and Environmental Care Foundation (HUDEFO), Sarah Pima, anasema kuwa kwa kushirikiana na wadau wengine wa mazingira, huwa wanafanya usafi katika ufukwe huo mara mbili kwa mwezi, wakikusanya taka, kuzitenga na kuzirejeleza.

Sara anabainisha kuwa kila wanaposafisha ufukwe huo, hukusanya wastani wa tani nne hadi 13 za taka ngumu. Kati yake, asilimia nane ni taka hatarishi za hospitalini.

"Kinachotusikitisha kila tunaporudi kusafisha ufukwe (kila baada ya wiki mbili), tunakuta kiwango kikubwa cha taka kana kwamba hakujafanyiwa usafi kwa muda mrefu," Sara anasema.

Vilevile, utafiti uliofanywa na Samwel Manyele na wenzake wa mwaka 2013, ukiangazia mifumo ya usimamizi wa taka za hospitalini katika vituo vya afya vya ngazi za chini (LLHF) katika wilaya za Ilala na Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, ulionesha kuwa asilimia 83 ya vituo vya kutolea huduma za afya katika Manispaa ya Kinondoni hufukia taka katika mashimo.

Watafiti hao pia walibaini zaidi ya asilimia 50 ya maeneo zinakotupwa taka hizo, hayakuwa na uzio na yalikuwa karibu na makazi ya watu.

"Asilimia 47 ya vituo vya afya katika wilaya za Ilala na Kinondoni hazina taratibu za uendeshaji wa kawaida wa usafirishaji taka za hospitalini. Ni changamoto kubwa zaidi katika Manispaa ya Kinondoni ambako asilimia 71 ya vituo vya afya hubeba taka hatarishi kwa mikono wakati wa kwenda kuzitupa, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira," inasomeka sehemu ya ripoti ya watafiti hao.

Licha ya angalizo hilo la miaka 12 iliyopita, mwandishi wa habari hii amefika kwenye ufukwe wa Rainbow, katika Manispaa ya Kinondoni na kukuta taka hatarishi, zikiwamo za hospitalini, zikiwa zimetapakaa pembezoni mwa ufukwe.

Taarifa ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliyochapishwa mwaka 2019, inabainisha kuwa mkoa huo huzalisha taka ngumu tani 4,600 kwa siku.

Hata hivyo, taarifa hiyo inabainisha kuwa ni asilimia 6.5 (tani 299) tu ndiyo hurejelezwa, hivyo kuziacha tani 4,301 (asilimia 93.5) zikitupwa ovyo mitaani, ikiwamo mito na hatimaye kuishia kwenye fukwe za bahari.