RIPOTI MAALUM: Gesi yageuka mateso kwa madereva magari na bajaji

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 10:19 AM Oct 03 2024
Bajaji zinazotumia gesi, zikiwa kwenye foleni ya kujaza nishati hiyo, katika eneo la Uwanja wa Ndege, jijini Dar es Salaam.
PICHA: JUMANNE JUMA
Bajaji zinazotumia gesi, zikiwa kwenye foleni ya kujaza nishati hiyo, katika eneo la Uwanja wa Ndege, jijini Dar es Salaam.

MOSHI wa magari yanayotumia mafuta unasababisha vifo vya watu 385,000 kila mwaka. Rai ya serikali ni wananchi waachane na matumizi ya mafuta, watumie gesi.

Lakini Tanzania hivi sasa ina vituo vitano tu vya kujaza gesi katika magari, vitatu vikiwa mkoani Dar es Salaam ambako madereva wa magari na bajaji wanakaa hadi saa nane kwenye foleni ya kujaza gesi, huku serikali ikikiri vituo vilivyoko vimeelemewa na wingi wa wahitaji.

Ni dosari changamoto iliyoibuka kipindi ambacho kuna mwitikio mkubwa wa wamiliki wa vyombo vya moto kutumia gesi ili kulinda mazingira.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe katika vituo vitatu vinavyotoa huduma hiyo mkoani Dar es Salaam; Ubungo, TAZARA na Uwanja wa Ndege, umebaini baadhi ya madereva wanapokwenda kituoni kujaza gesi, hukaa kwenye foleni zaidi ya saa nane hadi kupata huduma hiyo. Vituo vingine ni viwili vya kujaza gesi katika vyombo vya moto nchini, viko Mkuranga (Pwani) na Mtwara.

Thomas Samson dereva bajaji na mkazi wa Sinza, wilayani Kinondoni aliyekutwa kituo cha kujaza gesi Ubungo, anashauri huduma hiyo iwekwe katika kila kituo cha mafuta jijini.

"Kuna siku unakaa zaidi ya saa tano hadi nane kupata huduma kutokana na foleni. Sisi tunaofanya biashara ya usafirishaji, hali hii ni kupoteza muda wa kutafuta fedha. Kuna wakati unasema uje usiku wa manani, lakini napo pia unakutana na foleni," analalama.

Dereva huyo anasema baada ya kufunga mfumo wa gesi katika bajaji, gharama ya kujaza gesi ni Sh. 6,000 hadi Sh. 7,000, lakini anapata wastani wa kati ya Sh. 80,000 hadi Sh. 100,000 kutokana na matumizi ya gesi hiyo.

Dereva mwingine anayeegesha bajaji yake Magomeni, wilayani Kinondoni, Rashidi Bakari anasema:

"Katika vituo vya gesi vilivyoko Dar es Salaam vyenye uhakika ni cha Ubungo na Uwanja wa Ndege. Ukienda cha TAZARA wakati mwingine huduma hukosekana kwa sababu wao wanategemea gesi kutoka kituo cha Ubungo.

"Hakijaunganishwa na bomba la gesi kama kituo cha Ubungo lakini pia cha Uwanja wa Ndege angalau kina pampu sita za kujazia gesi, hivyo pale wanahudumia bajaji na magari mengi kwa wakati mmoja," anasema.

Martin Msafiri, mkazi wa Kigamboni, analalama kupoteza muda mwingi kwenye foleni ya kujaza gesi katika gari lake. Anataja adha hiyo ni kikwazo katika harakati zake za utafutaji (uchumi).

"Unakuta zaidi ya magari 100 yamekutangulia, unapoteza muda wote wa kuingia barabarani kutafuta ridhiki, inaumiza sana," anasema Msafiri.

Kiango Mgwale, aliyekutwa katika foleni kituo cha Uwanja wa Ndege, anasema alifika kituoni huko saa tano asubuhi, lakini hadi wakati huo (saa tisa alasiri) alikuwa hajapata huduma.

"Gesi ni rasilimali yetu wenyewe, lakini kuitumia ni tatizo. Serikali iangalie namna ya kuitawanya nchi nzima," anashauri.

Muuzaji wa gesi katika kituo cha Ubungo, Joe Chimazi, anakiri kituo kuelemewa na wateja kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi kwenye matumizi ya gesi, ukichangiwa na gharama zake kuwa ndogo kulinganisha na matumizi ya petroli na dizeli.

Anabainisha kuwa kwa siku wanahudumia zaidi ya bajaji na magari 1,000 yanayokwenda kupata huduma katika kituo hicho.

"Mfumo huu unawapa faida kubwa zaidi wenye magari makubwa, wanaweza kujaza gesi ya Sh. 100,000 wakaenda Iringa na kurudi na kwa kutumia mafuta, umbali huo ni zaidi ya Sh. 500,000," anasema.

Katika kituo cha TAZARA, Meneja Utawala Mary Aloyce, anataja changamoto kubwa ni kuishiwa gesi kunakotokana na idadi ya wahitaji wanaokwenda kupata huduma hiyo.

"Sababu kubwa ni kwamba, tunategemea gesi kutoka katika kituo cha Ubungo, hivyo wakati mwingine huwa tunaikosa na kusababisha wateja kusubiri kwa muda," anasema.

Mary anataja changamoto nyingine kituoni huko ni kuwapo bomba moja linalojaza gesi na kusababisha kushindwa kutoa huduma haraka kwa wateja.

Julai 29 mwaka huu, saa nane mchana, mwandishi wa habari wa Nipashe alizuru kituoni huko. Huduma ilikuwa imesitishwa, lakini aliona wateja waliosema walikuwa wanasubiri gesi iliyofuatwa kwa gari kituo cha Ubungo.

Mwandishi pia alitembelea kituo cha Uwanja wa Ndege ambako Msimamizi wa Shughuli na Matengenezo, Levocatus Lameck, aliungana na wenzake wa TAZARA na Ubungo kwamba wameelemewa wateja kiasi cha kuwa na foleni ndefu za magari na bajaji vituoni.

"Bei ya gesi ni nusu ya ile ya mafuta. Kwa mfano, mtu anayetumia gari aina ya Toyota IST, Raum, Vits, akifunga mtungi wa gesi wa kilo 11, anaujaza kwa Sh. 17,000 na akatembea umbali wa kilometa 180 huku amewasha kiyoyozi.

"Hapa tunaongelea umbali wa kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ambapo kwa mafuta mtu huyo angetumia zaidi ya Sh. 120,000.

"Kwa bajaji mtu ambaye ana mtungi wa kilo nne na nusu, anatumia Sh. 6,800 kujaza, anaweza kutembea umbali wa Km 240. Unaweza kuona mtu kama huyo ni kwa namna gani anaokoa fedha nyingi, ni mara mbili ya kiwango ambacho angeweza kutoa," anafafanua.

Lameck anasema kwa takwimu ambazo si rasmi, kuna zaidi ya bajaji 3,500 zenye mfumo wa gesi ambazo kwa siku wao huhudumia zaidi ya bajaji 600 na magari zaidi ya 1,000.

Anasema kuwa kituo hicho kina pampu sita zinazohudumia magari sita kwa dakika nne hadi tano.

"Tuna mikonga ya kujazia gesi sita, hivyo kwa mara moja tunajaza katika vyombo sita na presha yake ni kubwa. Ninashauri kama vikijengwa vituo vingine, viige mfumo wetu huu," Lameck anasema.

HATUA SERIKALINI

Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Gesi na Mafuta wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Emmanuel Gilbert, anakiri vituo vya kujaza gesi mkoani Dar es Salaam kuelemewa na wingi wa wahitaji wa nishati hiyo.

Anasema msongamano mkubwa unaoshuhudiwa hivi sasa vituoni umetokana na kuongezeka kwa uelewa wa matumizi ya gesi asilia na gharama ndogo kulinganisha na matumizi ya mafuta.

Anasema kuwa awali wananchi walikuwa wanasita kutoka na ugeni wa teknolojia, akiwa na ufafanuzi kuwa, "teknolojia ikiwa mpya, watu wengi huwa wanakuwa na wasiwasi kidogo, nini kinaweza kutokea, pia usalama upoje." 

Gilbert anasema tayari serikali imeona tatizo na imeshaanza kuchukua hatua na matokeo yameanza kuonekana.

"Kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya Mwaka 2015, gesi ilikuwa ni haki ya TPDC pekee, lakini serikali ikaona TPDC peke yake haina uwezo wa kusambaza huduma hiyo nchi nzima kutokana na mwamko wa watu na uhitaji kuwa mkubwa kutumia gesi asilia katika magari yao na bajaji.

"Kutokana na hali hiyo, tuliamua kutanua wigo kwa kuita wawekezaji binafsi na tayari kwa sasa wapo ambao wameshaanza kuwekeza," alisema.

Katika hilo, Gilbert anasema kituo cha Uwanja wa Ndege kilichozinduliwa Desemba mwaka jana, ni cha kampuni binafsi na kinafanya vizuri na ndicho tegemeo zaidi hivi sasa kutokana na uwezo wake wa kujaza magari sita kwa wakati mmoja.

"Sasa kampuni hiyo hiyo ina mpango wa kujenga kituo kingine barabara ya Sam Nujoma, halafu sisi TPDC tunajenga kituo kikubwa maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jirani na Hosteli za Dk. John Magufuli kitakachowezesha kutoa gesi kutawanya katika vituo vingine," anasema.

Anakitaja ni kituo hicho ambacho kitaleta ushindani katika soko kwa kuwa kitakuwa na uwezo wa kusambaza gesi kwa vituo vidogo ambavyo havijaunganishwa na miundombinu ya gesi asilia.

"Isivyo bahati, kituo cha Ubungo kimefikia mwisho, hakina uwezo wa kutoa gesi kwenda kwenye vituo vinavyotarajiwa kujengwa, hivyo huduma hiyo itaanza kupatikana Desemba mwaka huu tutakapomaliza ujenzi wa kituo cha TPDC na kitakuwa na uwezo mkubwa kuliko cha Ubungo.

"Pia tuna uhakika gesi inaweza kutoka pale ikafika Morogoro, Tanga na Dodoma na katika mikoa mingine itategemeana na wawekezaji watakavyochangamkia fursa," anasema Gilbert.  

*ITAENDELEA KESHO