Rais Samia kuhudhuria shindano la dunia kusoma Quran Tukufu

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 02:55 PM Feb 18 2025
Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakari Zuberi, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ofisi za Makao Makuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA). Kushoto ni Mwakikishi wa Balozi wa Saudi Arabia, Shekhe Mutabi Bin Suleiman.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakari Zuberi, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ofisi za Makao Makuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA). Kushoto ni Mwakikishi wa Balozi wa Saudi Arabia, Shekhe Mutabi Bin Suleiman.

RAIS Samia Suluhu Hassan, anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye mashindano ya dunia ya kusoma Quran Tukufu, yatakayofanyika nchini katika Uwanja wa Benjamini Mkapa Februari 23, mwaka huu.

Akizungumza na vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam, Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakari Zuberi, amesema kuwa mashindano hayo yanatarajia kushindanisha mabara matano, Afrika, Asia, Arabu na Ulaya.

Amesema hayo ni mashindano ya kwanza kuhudhuriwa na mabara mengi, kwa kuwa inatokana na sera na juhudi za Rais Samia, kuimarisha urafiki na undugu pande zote za dunia.

Aidha alitoa wito kwa wazazi kujikita kwenye malezi bora, yakiwamo kuwaelekeza watoto kwenye elimu ya dini, ili kuwe na taifa bora na makini lenye kumuogopa Mungu, kwani dini ndio mwongozo wa maisha.

Mwakilishi wa Balozi ya Saudi Arabia, Shehe Mutab Bin Azamay Suleiman, amesema wanaushukuru uongozi wa Tanzania unaoongozwa na Rais Samia, kuwa nchi ya mfano yenye utulivu na amani hadi mashindano hayo makubwa kufanyika nchini.

Mwandaaji wa Mashindano hayo ya Dunia, Shehe Othuman Kaporo, akisisitiza jambo mbele ya vyombo vya habari
Amesema tayari Waziri Mkuu wa Saudi Arabia ameshasaini mikataba ya kusaidiana kati ya BAKWATA na serikali ya Saudi Arabia na matunda yameaanza kuonekana, kwa makubaliano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Mwandaaji wa Mashindano hayo, Shekhe Othuman Kaporo, amesema mashindano yataongozwa na kuhudhuriwa na Imam Mkuu wa Msikiti wa Saudi Arabia wa Madina, Shekhe Abdallah Buaijan, na kwa mara ya kwanza Tanzania kupata ugeni huo.

Amesema washiriki wataweza kujinyakulia zawadi mbalimbali, zikiwamo magari, bajaji, pikipiki na tiketi za kwenda kuhiji Mji Mtakatifu ‘Mecca’.

Pia wahudhuriaji watakaofika katika Uwanja wa Benjamini Mkapa wataweza kuangalia na kupima afya zao bure, kwa magonjwa yasiyoambukiza.