Rais Samia ahimiza Afrika ijipange

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:59 AM Feb 17 2025
Rais Samia Suluhu Hassan
Picha: Mtandao
Rais Samia Suluhu Hassan

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewasilisha Azimio la Dar es Salaam na kueleza kwamba Afrika inapaswa kuendelea kushiriki kikamilifu kutetea maslahi na kuhahakisha inapanga mbinu mpya kutumia rasilimali mabadiliko ya tabianchi.

Samia alisema hayo baada ya kushiriki katika kikao cha pembezoni cha Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSSCC).

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga, ameeleza hayo katika taarifa kwa umma, iliyotolewa Februari 16, mwaka huu.

Pia, pamoja na mambo mengine, Rais Samia, amewashukuru wakuu wa nchi, kwa kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati Afrika wa Misheni 300, uliofanyika jijini Dar es Salaam. 

Akieleza zaidi, katika kikao hicho, kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CAHOSSC, Rais wa Kenya, William Ruto, Rais Samia amewasilisha Azimio la Dar es Salaam na kueleza kuwa Afrika, inapaswa kuendelea kushiriki kikamilifu kwenye majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi.

Wakuu wa nchi za Afrika
Akipokea Azimio hilo, Rais Ruto, amempongeza Rais Samia, kwa kufanikisha Mkutano wa Misheni 300 na Kkikao kiliridhia Azimio hilo, kuwasilishwa kwenye Baraza la Umoja wa Afrika, kwa ajili ya kupitishwa na Baraza hilo.  

Aidha, Baraza lilipitisha Azimio hilo bila kupingwa. 

Rais Samia alipata fursa ya kuwasilisha ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, iliyopendekezwa na Tanzania katika Baraza la Umoja wa Afrika na ameeleza nishati hiyo ni hitaji muhimu kwa watu milioni 900 barani Afrika.

Baraza hilo limemtambua na kumpongeza Rais Samia kama Kinara wa ajenda hiyo, barani Afrika.

Awali, tarehe Februari, 15, 2025, Mkutano wa Kawaida wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliichagua Tanzania kuwa mjumbe wa Kamati ya Uongozi wa Umoja wa Afrika (Bureua of the African Union Assembly), kwa mwaka 2025.

Kamati hiyo inaundwa na Angola kutoka Kanda ya Kusini (Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika 2025); Burundi kutoka Kanda ya Kati (Makamu wa Kwanza wa Mwenyekiti); Ghana kutoka Kanda ya Magharibi (Makamu wa Pili wa Mwenyekiti) na Tanzania kutoka Kanda ya Mashariki (Makamu wa Tatu wa Mwenyekiti).

Aidha, Mauritania iliyokuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, kwa mwaka 2024 kutoka Kanda ya Kaskazini itakuwa Katibu wa Kamati hiyo.