Ole Sendeka afunguka kiini cha risasi 18

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 10:49 AM Apr 03 2024
Mbunge wa Simanjiro, mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka (kulia) akizungumza  na Mbunge wa Afrika Mashariki, James Ole Millya wakati wa mkutano wa hadhara jimboni humo juzi. Wa (pili kushoto) ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Simanjiro, Baraka Kanunga.
PICHA: NA MWANDISHI WETU
Mbunge wa Simanjiro, mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka (kulia) akizungumza na Mbunge wa Afrika Mashariki, James Ole Millya wakati wa mkutano wa hadhara jimboni humo juzi. Wa (pili kushoto) ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Simanjiro, Baraka Kanunga.

MBUNGE wa Simanjiro (CCM), mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka, amefichua kile kilichojificha nyuma ya pazia kuhusu kushambuliwa na risasi akisema siku moja kabla ya tukio hilo alifanya mazungumzo na viongozi wa juu, kuhusu hatma ya ardhi ya wafugaji inayotakiwa kubadilishwa kuwa maeneo ya hifadhi.

Ole Sendeka akiwa safarini alishambuliwa kwa risasi Machi 29 mwaka huu majira ya saa 12:45 jioni katika Kijiji cha Ngabolo, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Simanjiro, Ole Sendeka, amesema Alhamisi ya Machi 28 mwaka huu alikaa na viongozi kujadili suala la kupandishwa hadhi kwa mapori ya wafugaji.

“Niwape na siri nyingine. Ijumaa ndiyo nimeshambuliwa (Machi 29), Alhamisi (Machi 28), nilikaa na viongozi kujadili kupandishwa hadhi kwa mapori haya ya wafugaji. Tena viongozi wa ngazi za juu kabisa. Na tukaelewana, kila mmoja anasema hatutakubali ardhi yetu ibadilishwe kuwa ardhi ya wanyama. wamesema wenyewe.

“Lakini hii hainifanyi nisiende bungeni kusema. Ngojeni niwaambie, hotuba yangu ya kwanza bungeni haitakuwa kueleza kupigwa kwangu risasi.

…Itakuwa ni kueleza kwamba ardhi ya wafugaji wa Simanjiro, ardhi ya wafugaji wa Monduli, ardhi ya wafugaji wa Ngorongoro, ardhi ya wafugaji wa Longido, ardhi ya wafugaji wa Kiteto, ardhi ya wafugaji wa Same na Mwanga; wamependekeza nazo ziwe hifadhi katika ardhi wanazoishi wamasai.”

Katika mkutano huo, Ole Sendeka, amesema atakwenda kueleza kwamba serikali ikichukua hata kilomita moja katika eneo hilo, kwa ajili ya kisingizio cha uhifadhi ni kuweka rehani maisha ya wafugaji walioko hapo, kwa sababu wafugaji watakuwa hawana maisha tena.

“Walitaka kuniondoa uhai ili niache watoto wangu wadogo. Nina uhakika serikali haina mkono katika jaribio la kutaka kuondoa maisha yangu. Wangehusika ningemtaja mmoja hadi mwingine kwa jina. Naomba tuelewane, serikali ya CCM (Chama Cha Mapinduzi) ingehusika, ningemtaja kwa jina hadharani.

Zaidi ameongeza: “Kazi iliyonayo serikali kwa sasa ni kuchunguza na kuwapata waliohusika. Wanaweza kuwa wana CCM wamefanya hilo, wanaweza kuwa watu wengine wa aina yeyote, lakini akiwa ni anayefanya kazi serikalini, akiwa ni wa upinzani, atapatikana.”

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Machi 30 mwaka huu na Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Naibu Kamishna, David Misime, imeeleza kuwa Christopher Ole Sendeka na dereva wake (ambaye hakutajwa jina) wakiwa safarini, gari walilokuwa wanatumia lilishambuliwa kwa risasi; na kwa bahati nzuri hakuna aliyepata madhara.

Kwa mujibu wa DCP Misime, polisi wanafuatilia tukio hilo kwa ukaribu sana, kwani uchunguzi ulishaanza baada ya kupokea taarifa, huku akisisitiza baada ya uchunguzi wa wataalam taarifa kamili itatolewa.