Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Deogratius Ndejembi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kulinda na kusimamia haki za watu wenye ualbino nchini ili kuwezesha kundi hilo kuwa na ustawi mzuri.
Ndejemni ametoa kauli hiyo leo alipokutana na Wabunge wa Viti Maalum kundi la watu wenye Ulemavu, Viongozi wa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) pamoja na Foundation for Disabilities Hope (FDH) kwa lengo la kujadili na kufuatia tukio la kuibwa mtoto mwenye Ualbino lililotokea katika Kata na Tarafa ya Kamachumu Wilayani Muleba, mkoani Kagera.
Aidha, Ndejembi amebainisha kuwa Utaratibu wa kulinda Watu wenye Ulemavu katika ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Kata na Wilaya utaendelea kutekelezwa kwa lengo la kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wote.
Amewataka Watu wenye Ulemavu kutokuwa na hofu kwa kuwa Vyombo vya Ulizi na Usalama vitaendelea kudhibiti vitendo hivyo na kuwachukulia hatua kali za kisheria watakao bainika kufanya matukio hayo.
Naye, Mbunge wa Viti Maalum, Stella Ikupa ameishauri Serikali kuwa na mpango na mikakati endelevu ambayo itaweza kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya Watu wenye Ulemavu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED