Myinga afafanua mgombea CHADEMA aliyeenguliwa kushinda uwenyekiti Usari

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 02:09 PM Dec 05 2024
Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Dionis Myinga.

HATIMAYE Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Dionis Myinga, amejitokeza kutoa ufafanuzi wa kile kinachoelezwa kuwa sintofahamu ya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Ritte aliyeenguliwa kwa pingamizi, kutangazwa kuwa mshindi na Mwenyekiti halali wa Kijiji cha Usari, Kata ya Machame-Narumu.

Akitoa ufafanuzi huo leo, Disemba 5, 2024 kuhusu madai hayo, Myinga amesema jambo hilo limekuwa likipotoshwa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na uchaguzi uliofanyika.

Amesema ukweli ni kwamba, Ritte, alivyorejesha fomu alienguliwa na baada ya kuenguliwa, alikata rufaa kwenye Kamati Rufaa ya Wilaya; na baada ya kuikata alishinda rufaa hiyo na jina lake likarejeshwa na kuingia kwenye kugombea Uenyekiti wa Kijiji cha Usari.

“Hata hivyo, baada ya kugombea kimsingi alishinda. Sisi tulimtambua baada ya ushindi huo na alikuja kuapishwa. Sasa hivi ni Mwenyekiti halali wa Kijiji cha Usari,”amesema Msimamizi huyo wa Uchaguzi Hai. 

Kwa mujibu wa Myinga, Halmashauri ya Wilaya ya Hai, ilifanya uchaguzi huo katika maeneo makuu mawili, ambapo ni kwenye vijiji 62 na vitongoji 292.

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba 27 mwaka huu nchini kote, Ritte anayedaiwa kuenguliwa, kukata rufaa na kutojibiwa wala kupiga kampeni, alimsinda mpinzani wake kwa kupata kura428, huku Mwalimu mstaafu Stella Moshi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akipata kura 408.