MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, aliyekuwa mwalimu wa madrasa katika Msikiti wa Ushirika wilayani hapa, Abdala Selemani (37), baada ya kukutwa na hatia ya kumlawiti mwanafunzi wake wa kiume mwenye umri wa miaka 12.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Nasra Mwashee ambaye alisema mahakama imeridhika bila kuacha shaka na ushahidi uliotolewa kuhusu kitendo hicho ambacho ni kinyume cha kifungu cha sheria namba 154(1) (a) cha Kanuni za Adhabu iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Alisema adhabu hiyo itakuwa fundisho kwake na watu wengine wenye tabia ya kufanya vitendo hivyo vya kikatili kwa watoto kwenye jamii na kuongeza kuwa ukatili kwa watoto hasa ubakaji na ulawiti, vimekuwa vikitokea mara kwa mara kwenye wilaya ya Nzega na adhabu hizo zitakuwa ni fundisho kwa wengine
Awali, Wakili wa Jamhuri, Jenipha Mandago, aliiambia mahakama hiyo kwamba Selemani alitenda kosa hilo Oktoba 15, 2023 majira ya saa 10:00 jioni baada ya kuwekewa mtego kwa kuwa alikuwa akiwalawiti watoto mara kwa mara ambao alikuwa akiwafundisha elimu ya dini katika msikiti huo.
Alisema tukio la kumlawiti mtoto huyo wa miaka 12 mwanafunzi (jina na shule vinahifadhiwa) alilifanya eneo la chooni na kumsababishia mtoto huyo maumivu makali mwilini.
Mandago alidai kwamba kutokana na kosa alilolitenda, aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye nia na tabia kama hizo kwenye jamii, ambao wanawatendea vitendo vya kikatili watoto.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, mahakama hiyo ilitoa nafasi ya utetezi kwa Selemani iwapo itamtia hatiani na kuomba apunguziwe adhabu kwa kuwa ana familia ya watoto wanne na mke ambao wanamtegemea.
Hata hivyo, mahakama haikuridhika na utetezi huo, hivyo kumhukumu kwenda jela akatumikie kifungo cha miaka 30.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED