Mtafiti ahofia hatari sokwe mtu kutoweka

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 07:30 AM Jun 15 2024
Sokwe.
Picha: Mtandao
Sokwe.

MTAFITI wa sokwe mtu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Simula Maijo, amesema wanyamapori hao wako katika hatari ya kutoweka hivi sasa kutokana na uharibifu mkubwa wa makazi yao.

Uharibifu huo ni ule unaosababishwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu hasa kilimo, ufugaji na uanzishwaji wa makazi holela ya binadamu katika maeneo yao ya asili. 

Kwa mujibu wa Maijo, sokwe mtu ambao ni rafiki wa mazingira, kwa asilimia kati ya 60 na 80, chakula chao kikuu ni matunda. 

"Sokwe ni mnyama adhimu Tanzania, ambaye kwa asili anapatikana katika mikoa ya Kigoma (Gombe na Mahale), Mkoa wa  Katavi (Misitu ya Tongwe) na baadhi ya maeneo ya Rukwa (Kalambo).  

"Tanzania ina Sokwe katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, ambao siyo wa asili katika maeneo hayo. 

 "Kwa Tanzania Sokwe wanakadiriwa kuwa chini ya 2,500 kwa idadi. Na kati ya idadi hiyo, zaidi ya asilimia 75 wanapatika na kuishi katika maeneo ambayo yanapatikana nje ya Hifadhi za Taifa za Gombe na Mahale," alisema.   

Aidha, mtafiti Maijo alisema sokwe ni mnyama wa kipekee na mwenye umuhimu mkubwa katika mifumo Ikolojia wanayopatikana, hivyo kuna uhitaji wa dhati kuhakikisha wanyama hao wanahifadhiwa ili kudumisha uwiano wa ikolojia wanayopatikana na kuishi. 

Pamoja na mambo mengine, Maijo alisema sokwe ndiye mnyama pekee aliye na ufanano mkubwa  wa vinasaba na binadamu. 

Taarifa za kisayansi, zinaonyesha kuwa sokwe anashahabiana kivinasaba na binadamu kwa zaidi ya asilimia 98. 

Mtafiti huyo alifafanua kuwa katika uhifadhi, sokwe wanasaidia kusambaza mbegu mbalimbali kutokana na vyakula wanavyokula.  

Katika kula matunda ya mimea ambayo ni chakula chao, sokwe huwa wanameza pia mbegu za matunda hayo. 

Utafiti unaonyesha mbegu iliyopita katika mfumo wa umeng’enyaji wa chakula cha Sokwe ina asilimia kubwa ya kuota ikilinganishwa na mbegu ambazo hazikupitia mfumo huo. 

Akizungumzia upande wa uchumi, Mtafiti Maijo alisema sokwe wanachangia pato la taifa kupitia utalii wa picha.