Makonda aituliza BAKWATA hoja kupatiwa eneo la wazi

By Cynthia Mwilolezi , Nipashe
Published at 11:29 AM Dec 10 2024
Makonda aituliza BAKWATA hoja kupatiwa eneo la wazi
Picha: Mpigapicha Wetu
Makonda aituliza BAKWATA hoja kupatiwa eneo la wazi

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amemtaka Shekhe wa Mkoa huo, Shaaban Bin Jumaa kuwa na subira na ombi lake alilotoa kwa Rais Samia Suluhu Hassan la kupatiwa eneo la wazi la mnara wa Mwenge.

Amesema wanapaswa kuwa wavumilivu kwa kuwa suala hilo liko katika hatua za mwisho ili wakabidhiwe hati ya eneo hilo.

Akizungumza jana jijini Arusha wakati akihitimisha matembezi ya kuombea amani mkoa wa Arusha na taifa ikiwa ni maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makonda alionya kuwa asiwapo mtu yeyote akawapa hofu juu ya eneo hilo. 

"Shekhe wetu alimwomba Rais apewe eneo hili, ili waendeleze imani yao na akaniambia kuna jambo limekwama, ila leo (jana) ninapenda kusema Rais Samia alichoahidi kwa shekhe wetu kitatimia, asiwapo mtu akawapa hofu, taratibu zinaendelea.

"Na tayari nimemwona Waziri wa Ardhi, naye amenihakikishia anakamilisha mchakato na timu yake na atakapokamilisha tutakuja kukukabidhi hati. Maelekezo ya Rais wetu ni sheria. Ninaomba tuwe wavumilivu," alisema.

Makonda alisema kila mmoja anapaswa kurudi kwenye magoti ya Mungu, ili kila mmoja awe na maendeleo na kuepukana na mikosi na balaa.

"Ebu tuwe na muda wa kuomba na kila mmoja anapewa muda mwenyewe unatabiri mema katika maisha yako, ili adui anapotafuta hatia, yale maneno yanasimama katika maisha yako, halafu wewe kimbia maombi...

"Mimi sina uadui na mtu licha ya kuwa kuna wakati sikuwa na kazi miaka mitatu na miezi sita, niliishi bila mshahara na nikawajua watu, ila nimeweka agano kwa Mungu wangu tangu nilipopata uenezi mshahara wote niliweka madhabahuni mwa Mungu, hivyo ukichezea kiti unachezea kiti cha Mungu mwenyewe, utakutana na Mungu mwenyewe anayepokea mshahara wake," alisema na kuibua kicheko.

Makonda pia alisema mkesha wa mwaka mpya 2025 utafanyika kwenye mzunguko wa mnara wa Saa, jijini Arusha na nchi 12 zitashiriki kwa kula nyama na kunywa na ikitimu saa 5:40 usiku, watumishi wa Mungu watasimama kuongoza maombi hadi saa 6:00 usiku. 

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mariadhiano na Amani Tanzania (JMAT), Dk. Israel Ole Maasa alisema Makonda amechagua fungu jema, nalo halitaondolewa.

Shekhe  wa Mkoa wa Arusha, Shaaban Bin Jumaa aliombea nchi dhidi ya maadui wa ndani na nje ya nchi, ili vizazi vilivyopo na vijavyo viendelee kunufaika na amani iliyopo.

Laigwanani Mkuu wa Jamii Wamasai Tanzania, Isack Ole Meijo alimwombea Rais Samia na viongozi wote wa serikali afya njema.