TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imetoa matokeo ya uchunguzi wa malalamiko yanayohusu uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kuhusu viongozi kadhaa, akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.
Uchunguzi huo umehusisha malalamiko 14 ikiwamo dhidi ya Makonda, aliyelalamikiwa kutoa amri ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu mkazi wa mkoani humo kinyume cha utaratibu na sheria Juni, mwaka huu.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, akitoa taarifa ya uchunguzi wa malalamiko hayo kwa waandishi wa habari jana jijini hapa, alisema malalamiko 14 yaliyowasilishwa yamefanyiwa uchunguzi.
Alisema katika uchunguzi dhidi ya Makonda, THBUB imebaini kuwa amri iliyotolewa haikuwa halali na haikuzingatia aina ya makosa na utaratibu ulioainishwa kisheria wa utekelezaji wa mamlaka hayo.
“Na kwamba mwananchi huyo hakuwa mhusika wa madai ya msingi ambayo mkuu wa mkoa huyo aliyatumia kushughulikia suala lililokuwa mbele yake.
“THBUB imebainika kuwa pia, Makonda alivuka mipaka ya majukumu yake kwa kushughulikia na kutoa uamuzi katika suala ambalo lilipaswa kufuata mkondo wa kisheria wa kimahakama kwa kuwa madai hayo yangeshughulikiwa huko,” alisema.
Jaji Mstaafu Mwaimu alisema hata kama kulikuwa na viashiria vya makosa ya jinai, njia sahihi ingekuwa kulielekeza Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Kadhalika alisema pamoja na mkuu huyo wa mkoa kuitwa mbele ya THBUB ili kuwasilisha utetezi wake alikaidi kufanya hivyo.
GEKUL
Mwenyekiti huyo alisema tukio lingine lililofanyiwa uchunguzi ni lile la aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul, aliyehusishwa na kuwaingiza chupa sehemu ya haja kubwa, Hashim Ally na Michael Isara.
Alisema baada ya uchunguzi kwa kuzingatia maelezo ya watu mbalimbali waliohojiwa na vielelezo ambavyo THBUB ilivipata haikubaini suala hilo kufanyika.
“THBUB ilibaini kuwa walalamikaji walizuiliwa kwa muda mrefu wakati wakihojiwa na mlalamikiwa kuhusu tuhuma za kutaka kumwekea sumu Pauline Gekul pamoja na kupeleka madawa ya kishirikina katika hoteli yake iitwayo Paleii Lake View na hivyo kusababisha walalamikaji kukosa haki yao ya kuwa huru” alisema.
Hata hivyo, alisema taarifa za uchunguzi zenye mapendekezo kwa kila uchunguzi uliofanyika zimewasilishwa katika mamlaka husika kwa ajili ya utekelezaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED