WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wagombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) hawatakuwa na kazi kubwa kwa kuwa wataingia katika uchaguzi wakiwa na rekodi thabiti ya utekelezaji ilani ya chama.
Akizungumza katika mkutano wa CCM Jimbo la Maswa, mkoani Simiyu jana, Majaliwa alisema kuwa katika kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi, chama hicho kitaendelea kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana.
Alisema suala hilo litafanyika kimkakati ili wagombea wa chama hicho kwa ngazi ya urais na wabunge wasiwe na kazi kubwa ya kueleza waliyoyafanya, badala yake wakipita majimboni watumie muda wao kuomba kura.
"CCM ni chama kikubwa, kinachopendwa na kinachoaminiwa, kina sera zinazotekelezeka, kikiahidi kinatekeleza. Wanamaswa, leo mpo hapa na mbunge wa Maswa Mashariki, anawaeleza yanayotekelezwa ili mgombea wetu atakapofika hapa, kazi yake iwe ni ndogo ya kuomba kura," alisema.
Majaliwa alieleza kuwa wakati wa kampeni, Mgombea Urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea mwenza wake, Dk. Emmanuel Nchimbi watafika Maswa kuzungumza na wananchi na kueleza mipango na mikakati yao kwa miaka mitano ijayo.
"Wakati wa kampeni, Rais Samia na mgombea mwenza wake Dk. Nchimbi watakuja Maswa kuomba ridhaa yenu. Tunataka kazi yao iwe nyepesi kwa sababu tayari mmeona kazi nzuri iliyotekelezwa hasa katika kusogezea wananchi huduma kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo," alisema Majaliwa.
Alieleza kuwa Rais Hussein Ali Mwinyi ambaye ni mgombea urais wa Zanzibar, ataendelea na kampeni zake visiwani humo, huku chama kikiendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha maendeleo yanafika kila kona ya nchi.
Mbunge wa Maswa Mashariki ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, alisema jimbo hilo limepata fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema katika sekta ya afya, kumetekelezwa ujenzi wa vituo vya afya, ununuzi wa vifaa tiba na ujenzi wa hospitali, akitolea mfano Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambayo ilipata zaidi ya Sh. milioni 300 iliyofanikisha ujenzi wa jengo la kupokea wagonjwa wa dharura na kununua vifaa.
Alisema serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za elimu, maji na afya ili kuboresha maisha ya wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED