Majaliwa ataka CAG apewe uhuru

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 06:32 AM Apr 20 2024
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu, Kasim Majaliwa, amesema bila uhuru, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hawezi kutimiza ipasavyo wajibu wake wa kuhakikisha uwazi na uwajibikaji vinakuwapo katika matumizi ya fedha za serikali.

Amesema nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), zinapaswa kutambua maeneo yanayostahili kutiliwa mkazo baina ya serikali, Bunge, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi za Ukaguzi na Mabunge kwenye nchi za SADC (SADCOPAC).

Kauli hiyo aliitoa jana wakati akifunga Mkutano wa Kujenga Uelewa wa Pamoja na Ufanyaji wa Kazi wa Taasisi za Ukaguzi na Mabunge kwenye nchi za SADC (SADCOPAC), uliofanyika Zanzibar.

Majaliwa alisema miongoni mwa maeneo hayo ni kuunga mkono uhuru wa Ofisi ya CAG.

“Bila uhuru, CAG hawezi kutimiza wajibu wake ipasavyo katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji wa fedha za serikali. Kwa hiyo, wadau wote wanawajibika kulinda uhuru huu kupitia hatua za kisheria na msaada wa taasisi zenu,” alisema.

Alisema suala la kuimarisha uhusiano kati ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (AG) na Bunge ni la muhimu, kwa kuwa linasaidia kurahisisha utendaji kazi baina yao.

“Ushirikiano kati ya vyombo hivi unawezesha utendaji na usimamizi rahisi. Unaruhusu uchunguzi mzuri zaidi wa matumizi ya fedha za serikali. Ushirikiano huu unaweza pia kuboresha utawala na uwajibikaji ndani ya nchi wanachama,” alisema.

Majaliwa aliwataka washiriki wa mkutano huo waweke kipaumbele kuboresha utawala bora na uwajibikaji kwenye nchi zao.

“Kupitia hatua za kisheria na usimamizi, tunapaswa tuhakikishe kuwa, mifumo iko sawa na inaweza kuziwajibisha taasisi za serikali kupitia matumizi yao. Kwa kuzingatia haya, tunaweza kukuza uaminifu katika mifumo yetu ya utawala na ustawi wa raia wetu,” alisema.

Katika kusisitiza ushirikiano wa kikanda, Majaliwa aliwaambia washiriki wa mkutano huo kwamba, ushirikiano baina ya SADCOPAC na washirika wa kikanda unapaswa kuendelezwa na kuwaahidi kuwa, Tanzania ikiwamo Zanzibar zimejipanga kikamilifu kufanya kazi bega kwa bega na washirika hao ili kuboresha shughuli za ukaguzi kwenye ukanda huo.

Alisema serikali imejitolea kusaidia Taasisi Kuu za Ukaguzi (Supreme Audit Institutions), Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PACs) na wadau wengine muhimu ili kuhakikisha kunakuwa na matumizi bora na ya uwazi ya rasilimali za umma, njia ambayo inakuza utawala bora.

Awali, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, Mudrik Ramadhani Soraga, alisema Tanzania imefaidika kiuchumi na kimkakati kutokana na mkutano huo kufanyika nchini.

Alisema wabunge na wawakilishi waliokutana wamejadili mada ambazo zitawawezesha kusaidia serikali zao katika nchi za SADC kuimarisha uwajibikaji na matumizi mazuri ya rasilimali na mapambano dhidi ya rushwa.

“Lakini, nikiwa waziri mwenye dhamana ya utalii, mkutano huu umetuongezea mapato,” alisema Soraga.

Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Dk. Othman Abbasi Ali, ambaye ofisi yake ilikuwa mwenyeji wa mkutano huo, alisema mbali na kuimarisha ushirikiano, mkutano huo umetoa fursa kwa wajumbe wa PAC katika mabunge kubadilishana uzoefu wa njia bora za kufuatilia matumizi bora ya fedha za serikali katika nchi zao.

Mbunge kutoka Malawi na Mweka Hazina wa SADCOPAC, Mark Botomani, aliwashukuru marais, Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuweka mazingira mazuri yaliyowezesha mkutano huo kufanyika kwa usalama na kwamba, Tanzania imekuwa mshirika muhimu wa Jumuiya ya SADC.

Kwa niaba ya wajumbe wenzake wa SADCOPAC, Botomani ameahidi kuwa watafanyia kazi mambo yote waliyojifunza katika mkutano huo ambao awali ulifunguliwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Mwinyi.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia, wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na taasisi za ukaguzi kutoka nchi za SADC.