Kikokotoo, ripoti ya CAG, katiba kutawala maandamano CHADEMA

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 08:25 AM Apr 19 2024
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe akiwa na Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu.
PICHA: MAKTABA
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe akiwa na Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, wamepanga kutawanyika katika mikoa 14 kuendesha awamu nyingine ya maandamano kuanzia Aprili 22 hadi 30, mwaka huu, huku ajenda ya kikokotoo ikitawala maandamano hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, amesema mikoa ambayo viongozi hao wataongoza maandamano hayo ni Kanda ya Serengeti yenye mikoa ya Shinyanga, Mara na Simiyu.

Mingine ni Kanda ya Victoria yenye mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza na Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Arusha, Tanga, Manyara na Kilimanjaro. Pia amesema watakwenda Kanda ya Kati yenye mikoa ya Singida, Dodoma na Morogoro.

Ametaja baadhi ya ajenda zitakaongoza maandamano hayo ni pamoja na Kikokotoo cha mafao ya wastaafu, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), Katiba mpya na athari za mvua. 

"Kwa hiyo awamu ya kwanza itakayoanza Aprili 22, tutaanzia kanda hizo nne na viongozi wakuu wa chama wataongoza maandamano hayo,” amesema Mrema.

Amesema Aprili 22, Mbowe ataongoza maandamano Bukoba na siku inayofuata  atakwenda Kahama mkoa wa Shinyanga kisha Aprili  24 Geita mjini na 25 Bariadi na baadaye Musoma mjini Aprili 26.

Amesema Aprili 27 ataongoza maandamano Mwanza wilaya ya Sengerema, Aprili 29 ataongoza maandamano mkoa wa Tanga na Aprili 30 mkoa wa Kilimanjaro.

Kuhusu Makamu Mwenyekiti Lissu, amesema ataanzia Kanda ya Kaskazini Aprili 25 mkoani Arusha, Aprili 26 Manyara siku inayofuata  27 Singida mjini kisha Aprili 29 Dodoma mjini na kumalizia Morogoro Aprili 30.

Kwa mujibu wa Mrema, mbali na mikoa hiyo, huenda wakagusa na mkoa wa Katavi katika awamu hiyo kutokana na maandalizi ambayo yamefanywa kwenye mkoa huo.

"Kwa hiyo tutakuwa na misafara miwili na tumeshalijulisha Jeshi la Polisi katika maeneo hayo kutakakofanyika maandamano,” amesema Mrema.

Akizungumzia msimamo wa CHADEMA kuhusu kikokotoo, Mrema amesema wanachotaka ni serikali kutumia utaratibu wa zamani wa kuwalipa wastaafu mafao yao yote na kuachama na kanuni ya asilimi 33 wanayoitumia katika kikokotoo kipya.

"Msimamo wetu kuhusu kikokotoo ni kwamba, fomula waliyotumia ya kuwalipa wastaafu asilimia 33 ya mafao yao ni mbaya kwa sababu inawaumiza,” amesema Mrema. 

"Wako wastaafu ambao tunafahamu wanakaa kwenye makambi na hawa ni askari polisi, wanajeshi ambao unapompatia hiyo asilimia 33, hajajenga hata kibanda kwake na alitegemea mafao hayo ndio akajenge, leo ukimpatia hiyo hawezi kujenga na anaondolewa kambini,” amesema.

Mrema amesema ni vyema wastaafu wakapewa mafao yao yote badala ya kuwapatia kidogokidogo. 

“Hizo ni fedha za mfanyakazi ambazo aliwekeza kidogokidogo kwa kukatwa kwenye mshahara wake, kwa nini wakati wa kutumia serikali impangie, eti inasema ukiwapa zote zinaisha haraka, kwani wamekuja kukulalamikia kwamba zimeisha, wapeni haki yao kama ilivyokuwa kabla ya hiki kikokotoo kipya,” amesema Mrema. 

"Watumishi wanaokaribia kustaafu kwenye ofisi za umma, kila mmoja anapambana apate chochote kitu ili akistaafu asidhalilike mtaani. Hizi  ofisi hazikaliki watu wanahangaika kuandika madokezo ya programu na safari kwa sababu wanajua wanastaafu. Kwa hiyo tunaandaa utumishi wa umma ambao haufanyi kazi zake vizuri kwa sababu ya hofu ya kustaafu,” amesema.