KIFO CHA KIBAO; Lissu: Vyombo vya dola vichunguzwe kimataifa

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 11:01 AM Sep 12 2024
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu
Picha:Mtandao
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu

TAASISI mbalimbali zimeendelea kutoa matamko kulaani kuuawa kwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ally Kibao, huku Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu, akisema vyombo vya usalama havipaswi kuchunguza matukio ya utekaji, utesaji na mauaji.

Pia amesema vyombo hivyo vya usalama havitakiwi kuchunguza kwa kuwa vinashutumiwa jambo ambalo halitaweka imani kwa wananchi.

Lissu alishauri kuundwa  timu ya wataalamu wa kimataifa ambao hawajaegemea upande wowote kufanya uchunguzi huo.

Akizungumza na Jambo TV katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA), baada ya kuwasili kutoka Ubelgiji, Lissu alisema utaratibu unaofaa katika uchunguzi huo ni kuleta timu za kimataifa na si polisi kujichunguza.

Kauli ya Lissu imekuja zikiwa ni siku nne tangu Rais Samia Suluhu Hassan kuliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi juu ya kifo cha Kibao na kupewa taarifa za kina juu ya tukio hilo.

Rais alisema Tanzania inaongozwa na misingi ya kidemokrasia,  hivyo kila raia ana haki ya kuishi na serikali haitavumilia vitendo vya kikatili vya namna hiyo.

Lissu alisema vyombo vya usalama vinahitaji kuchunguzwa na kusafishwa ili vitekeleze majukumu ya kuimarisha ulinzi na usalama inavyostahili na si kujichunguza.

Alisema njia pekee inayofaa kutumika ni kuleta timu ya kimataifa kuchunguza matukio hayo kwa kuwa hao ni watu wanaoaminika kuitenda kazi hiyo vizuri bila kuegemea upande wowote.

“Idara ya Usalama wa Taifa  anayoiongoza mwenyewe (Rais Samia), Jeshi la Polisi ndio watuhumiwa wa kwanza. Watajichunguzaje? Lini Jeshi la Polisi limeshawahi kuchunguza chochote cha mambo haya?” alihoji.

Alisema utaratibu wa kuundwa kwa Tume ya Kijaji ya Uchunguzi ni mzuri ingawa changamoto yake ni kuwa tume hiyo inaripoti kwa rais na matokeo yanakuwa siri hivyo njia hiyo haifai kutumika.

JAJI AUNGA MKONO 

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa haki za binadamu, Jaji (mstaafu)  Thomas Mihayo, alishauri kuanzishwa kwa Mahakama Maalumu ya Uchunguzi itakayokuwa na mamlaka kamili ya kuchunguza matukio hayo kwa kina badala ya tume ya uchunguzi.

Alisema chombo hicho kitakuwa na nguvu zaidi kuliko tume ya uchunguzi kwani itaweza kukusanya na kuhoji mashahidi, na kutoa maamuzi yenye msingi wa kisheria.

Jaji Mohayo alisema tume za uchunguzi mara nyingi hazina mamlaka kamili na zinategemea ripoti zao kuwasilishwa kwa vyombo vingine vya dola, hali inayoweza kuchelewesha haki na kusababisha matokeo yasiyofaa.

KAULI YA MISA- TAN

Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-TAN), ililaani vikali  wimbi linaloendelea la utekaji wa mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia nchini hasa tukio la utekwaji na mauaji ya kada huyo wa CHADEMA.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Bodi ya Uongozi wa Taasisi hiyo, matendo hayo ni kielelezo tosha cha uvunjwaji mkubwa wa sheria na ukiukwaji wa haki za binadamu na hasa haki ya msingi ya kuishi.

Aidha, waliiomba serikali kuchukulia kwa uzito wimbi hili na kutengeneza mikakati mahususi ya kiuchunguzi, ikiwamo kuunda tume huru ya kijaji ili kufuatilia mwenendo huu haramu katika nchi hiyo.

“Jambo hili la utekaji na mauaji ambao yanafanywa kwa wanasiasa, wafanyabishara na raia wengine yanatengeneza chuki miongoni mwa wananchi na kunyooshewa vidole vyombo vya dola kama Jeshi la Polisi kuhusika na hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya matukio yamehusisha taasisi hiyo ya ulinzi hapa nchini,” iliisema taarifa hiyo.

Pia iliisihi serikali kuchukua hatua hizo kwa haraka iwezekanavyo ili kutoruhusu uharibifu mkubwa kuendelea kwenye jamii hasa nchi inapoelekea kwenye matukio makubwa ya kidemokrasia ya uchaguzi wa serikali za mtaa Novemba, mwaka huu na uchaguzi mkuu 2025.

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimeunga mkono hoja ya kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza matukio hayo ili kupata suluhu ya kudumu kwa lengo la kurejesha imani ya wananchi juu ya uhuru wao na haki za msingi za kikatiba ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi ambayo sasa iko mashakani.

Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi, alisema chama hicho kinatoa wito Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camilus Wambura na Mkuu wa Mafunzo wa Jeshi la Polisi wawajibike.

Aidha, alilitaka  Jeshi la Polisi lihakikishe kamba linatoa taarifa sahihi kwa umma dhidi ya watu wote waliochukuliwa na kutekwa kinyume na sheria kwa kueleza taratibu walizochukua mpaka kuhakikisha watu hao wanapatikana.

Alimtaka IGP atoe tamko la kuvunjwa kwa vikosi kazi vyote vilivyoundwa ambavyo vimekuwa vikifanya kazi kinyume na sheria za nchi.

Mzee Kibao mwananjeshi mstaafu, alitekwa jioni ya Septemba 6 mwaka huu, maeneo ya Kibo Complex Tegeta, Dar es Salaam, na watu waliokuwa na silaha ambao waliwataka abiria kutosema lolote, kupiga picha za mnato na mjongeo wakati wakimshusha kwenye basi la Kampuni ya Tashrif akielekea nyumbani kwake Sahare mkoani Tanga.

Mwili wake ulikutwa maeneo ya Ununio, huku ukiwa na majeraha makubwa ikiwamo usoni.

WADAIWA KUTISHIWA MAISHA 

Wakati huo huo, TLS ilitoa taarifa jana jioni kuwa imepokea kwa masikitiko taarifa ya kutishiwa maisha kwa mawakili Tito Magoti, Peter Madeleka na Onesmo Ole Ngurumwa.

Taarifa ya TLS iliyotolewa na Mwabukusi, ilisema kuwa walipokea taarifa kutoka kwa mawakili hao na kwamba vitendo hivyo ni kinyume cha Katiba.

“TLS inachukua kwa uzito usalama wa maisha ya wanachama wake wote. Wakili ana haki ya kisheria ya kuzungumza na kutoa maoni yake bila vikwazo na ana haki ya uhuru kwa kutumia haki hii katika kuelimisha jamii kuhusu haki za raia na utawala wa sheria,” alisema.

“TLS inalaani vitendo vyovyote vinavyoashiria kutishia  au kufifisha utendaji wa mawakili katika kazi zao kama maofisa wa mahakama na majukumu mengine waliyonayo kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha Sheria ya Mawakili Tanganyika.

“Vitisho vyovyote kwa wakili au mawakili ni vitisho kwa muhimili wa mahakama, vitisho kwa waheshimiwa majaji na mahakimu. Kwa ustawi wa taifa letu, TLS inatoa wito kwa serikali kutoruhusu hata kidogo kwa chombo hiki muhimu na kikubwa nchini chenye jukumu mahsusi la kutafsiri sheria na kutoa haki kwa watu wote, kutishiwa.”