Kemikali kilimo zachochea saratani

By Restuta James , Nipashe
Published at 11:33 AM Apr 19 2024
Maabara ya kilimo.
Picha: Maktaba
Maabara ya kilimo.

WANAHARAKATI wa haki za binadamu wamesema matumizi yasiyo sahihi ya kemikali kwenye kilimo, yanachangia ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, saratani, figo na moyo.

Kutokana na hali hiyo, wanaharakati hao wameanzisha utafiti ili  kubaini ni kwa kiwango gani viuatilifu hivyo vinahatarisha afya za wananchi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Tanzania Relief Initiative (TRI), Wakili Edwin Mugambila, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa asilimia 70 ya vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza vinawapata watu kabla ya wakati.

“Moja ya visababishi vikubwa vya NCD ni ulaji usiofaa. Tumekuwa  mara kwa mara tukizungumzia matumizi ya sukari, chumvi, mafuta, pombe na tumbaku kama kichochezi lakini kuna tatizo kubwa ambalo ni kemikali zitokanazo na viuatilifu katika kilimo cha kisasa.

“WHO (Shirika la Afya Duniani) inasema hizi kemikali zinazotumika kwenye kilimo zinasababisha asilimia 25 ya vifo vyote vinavyotokea duniani kila mwaka yanayotokana na maradhi ya moyo, figo, saratani na kisukari. Njia hatari zaidi ni kemikali kuingia kwenye damu kwa kula vyakula vilivyolimwa kwa viuatilifu hatarishi.

“Unaweza kusema mimi situmii chumvi, sukari, mafuta, sinywi pombe wala sivuti sigara lakini utanunua nyama, karoti, kitunguu, mchicha au embe ambalo limelimwa kwa kemikali mbaya sana. Wataalamu  wanasisitiza tule mboga na matunda na lishe bora lakini kwa sasa hii ni hatari kuliko sukari,’ alisema.

Alisema baadhi ya kemikali zilizoko kwenye viuatilifu ni ‘carbosulfan’ inayotumika kudhibiti visumbufu kama wadudu wakiwamo mchwa, minyoo kwenye viazi, mpunga, mahindi na baadhi ya matunda.

Alitaja kemikali nyingine kuwa ni ‘diazinon’ inayotumika kuua mende, mchwa na jamii ya nzi kwenye majengo. Nyingine ni DDT ambayo ilipigwa marufuku baada ya kutumika kwa miongo mingi na kubainika kusababisha maradhi ya saratani. DDT pia inatumika kuangamiza mazalia ya mbu nchini.

Kemikali nyingine, alisema ni ‘endrin’ inayotumika kudhibiti visumbufu vya mazao kama panya na ndege waharibifu.

“Utafiti wa kitaalamu unatuambia kwamba kemikali hizi zinahusishwa kusababisha magonjwa kama saratani ya tezi dume, maini na damu, magonjwa ya moyo, ya sukari, ugonjwa wa kutetemeka, figo, kuzeeka na upumuaji. 

“Haya ni matatizo makubwa sana ambayo yanasababishwa na matumizi ya kemikali. Tumekutana hapa wataalamu kuzungumzia ukubwa wa tatizo hili na kutengeneza kwa pamoja mikakati ya kudhibiti madhara yatokanayo na viuatilifu,” alisema.

Mugambila alisema wanaharakati wanataka afya ya umma ilindwe katika nyanja zote ili kuipunguzia serikali na wananchi mzigo wa matibabu.

MZIGO MKUBWA 

Kwa mujibu wa Mugambila, Tanzania inatumia zaidi ya Sh. bilioni 99 kila mwaka kutibu magonjwa yasiyoambukiza na kwamba asilimia 13.2 ya vifo nchini vinatokana na maradhi hayo.

Alisema hivi karibuni, Malaysia ilifanya utafiti na kubaini kwamba miaka michache ijayo, asilimia 72 ya wakulima waliokuwa wanatumia viuatilifu vyenye kemikali hizo,  watapata maradhi ya saratani na moyo na kwamba matumizi ya kemikali yana madhara makubwa kwa siku zijazo.

“Sisi kama wadau tutawaandalia ushahidi wa hali ilivyo ili serikali ichukue hatua stahiki ikiwamo kutengeneza sera, sheria na miongozo ili kuwalinda Watanzania,” alisema.

Pia alisema takwimu za kimataifa zinaonyesha kwamba kila mwaka watu milioni moja hufariki dunia kwa magonjwa yasiyoambukiza duniani ambao asilimia 70 kati yao wanafariki kabla ya wakati.

“Asilimia 17.9 ya watu hufariki (dunia) kwa magonjwa ya moyo kila mwaka, asilimia tisa  kwa saratani, asilimia 3.9 magonjwa ya upumuaji na asilimia 1.6 kwa kisukari,” alisema.

Mhadhiri na Mtafiti wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Dk. Fredrick Mashili, alisema visababishi vya NCD ni vingi ikiwamo usalama wa vyakula.

“Tunapoongelea viuatilifu tunaangalia kemikali zinazotumika kwenye kilimo kama mbolea na dawa zinazopulizwa kwenye mazao kama matunda na mboga kwa ajili ya kuzuia wadudu waharibifu. Tunafahamu kemikali zikizidi kiwango zinakuwa na madhara katika mwili wa binadamu,” alisema.

“Nilipoongelea chakula kama matunda na mboga kuwa na kiwango kikubwa cha hizi kemikali ambazo zinaweza kusababisha haya magonjwa. Tumekutana hapa kuzungumzia kwamba kuna umuhimu wa udhibiti na kuhakikisha wadau wanazingatia viwango vinavyoruhusiwa kuwepo kwenye mazao ili kumlinda mlaji,” aliongeza. 

Alisema WHO inaelekeza kuwa baada ya matumizi ya kemikali kwenye kilimo, mazao yanapaswa kutumiwa baada ya muda fulani ili kupunguza madhara kwa walaji lakini hali ni tofauti kwa kuwa mengi yanafika sokoni yakiwa na kiwango kikubwa cha dawa.

Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA), Happy Nchimbi, alisema utafiti mwingi uliofanyika unaonyesha viuatilifu vinachangia  magonjwa yasiyoambukiza. 

Alisema matumizi ya kemikali kwenye kilimo hayakwepeki bali wananchi wanapaswa kuzitumia kwa usahihi.

Ofisa Viwango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Stephanie Kaaya, alisema shirika hilo linahakiki bidhaa zote za chakula zina usalama na ubora kabla hazijamfikia mlaji.

“Tunapima kiwango cha uatilifu kuhakikisha mabaki yako katika kiwango cha chini ambacho hakitamuathiri mlaji, tunapima pia kiwango cha chumvi, mafuta na protini ili kuona bidhaa zinakidhi kile kilichoandikwa,” alisema.

Naye mwanaharakati wa haki za binadamu, Wakili Wiliam Maduhu, alisema mnyororo wote wa mifumo ya vyakula unapaswa kuzingatia weledi ili mtumiaji wa mwisho asidhurike.

Kwa mujibu wa wanaharakati hao, utafiti wa WHO wa mwaka 2012 kwa kushirikiana na serikali, ulibaini kwamba asilimia tisa ya wananchi wanaishi na kisukari na asilimia 26 wana magonjwa ya moyo.

Juzi, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Magonjwa Yasiyoambukiza katika Wizara ya Afya, Dk. Omary Ubuguyu, alisema kuna ongezeko kubwa la magonjwa hayo nchini na chanzo kikubwa ni ulaji usiofaa huku takwimu zikionyesha kwamba watu saba pekee  kati ya 100 nchini wanazingatia mlo kamili.