TUCTA yaipongeza NBC udhamini maadhimisho Mei Mosi Arusha

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:40 PM May 02 2024
Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya NBC wakishiriki kwenye maandamano ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi ambayo kitaifa yalifanyika jijini Arusha jana. Maadhimisho hayo yaliyoongozwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.
Picha: Mpigapicha Wetu
Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya NBC wakishiriki kwenye maandamano ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi ambayo kitaifa yalifanyika jijini Arusha jana. Maadhimisho hayo yaliyoongozwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeungana na maelfu ya wafanyakazi kote nchini kusherekea Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi ambayo kitaifa yamefanyika jijini Arusha yakiongozwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango aliyemuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini humo, yalipambwa na uwepo wa washiriki wengi zaidi wakiwemo viongozi mbalimbali wa kiserikali, kidini, vyama na shirikisho la wafanyakazi huku Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na wakubwa wa benki hiyo, Elibariki Masuke akiwaongoza wafanyakazi wa benki hiyo kushereheka siku hiyo muhimu.

Akizungumzia maadhimisho hayo Masuke alisema mbali na ushiriki huo benki ya NBC ni miongoni mwa wadhamini wakubwa wa maadhimisho hayo yanayoratibiwa na Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali vikiwemo vyama mbalimbali vya wafanyakazi.

“Katika maadhimisho haya NBC tunaungana na maelfu ya wafanyakazi wenzetu kote nchini kusheherekea siku hii muhimu sana kwa wafanyakazi, kwanza tukiwa kama wafanyakazi, pili tukiwa wadhamini muhimu katika kufanikisha uratibu wa maadhimisho haya na zaidi tunashiriki kama watoa huduma za kifedha kwa wafanyakazi kupitia matawi yetu yaliyopo kote nchini,’’ alisema.

Kwa mujibu wa Masuke, benki hiyo imekuwa na utamaduni wa kudhamini maadhimisho hayo kwa miaka mingi sasa kutokana na kutambua umuhimu wake kwa wafanyakazi ambao ni nguzo muhimu katika ustawi wa benki hiyo kupitia huduma mbalimbali za kibenki inazozitoa kwa wafanyakazi hao.

“Ushirikiano wetu na wafanyakazi unaimarishwa zaidi na huduma zetu tunazozitoa mahususi kwao kwa kuzingatia mahitaji yao ikiwemo kuwatunzia amana zao kupitia akaunti mbalimbali kulingana na machaguo yao. Pia tunawapatia mikopo ya muda mrefu na mfupi bila dhamana na mikopo hiyo imekuwa na tija sana kwao kwa kuwa inawawezesha kujenga au kununua nyumba, kununua magari na vitendea kazi mbalimbali…na hiyo ndio tafsiri sahihi ya kampeni yetu ya ‘Shinda Mechi Zako Kinamna yako’ ‘’ alisema.

Zaidi Masuke alitumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wenzake wa benki ya NBC kwa namna wanavyotimiza majukumu yao kwa weledi, ubunifu na ufanisi wa hali ya juu hatua ambayo imekuwa ikiwavutia zaidi wateja wa benki hiyo wakiwemo wafanyakazi wa mashirika na taasisi mbalimbali wanaoitazama benki hiyo kama kimbilio muhimu katika huduma za kifedha.

Akizungumza kwenye Maadhimisho hayo Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya pamoja na mambo mengine aliwasilisha shukrani zake za dhati kwa taasisi fedha na wadau wengine ikiwemo benki ya NBC kwa jitihada zao katika kufanikisha maadhimisho huku akionesha kuguswa na mchango unaotolewa na taasisi hizo katika kuwahudumia wafanyakazi hao.