‘Jihadharini wanasiasa wenye lugha chochezi’

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 07:59 AM Jun 15 2024
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Mlata.
Picha: Mpigapicha Wetu
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Mlata.

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Mlata, amewataka wananchi kuwakataa viongozi wa kisiasa wanaotoa kauli za kichochezi, kibaguzi na zenye viashiria vya kuvunja amani nchini.

Akizungumza juzi na wananchi mjini Kiomboi wilayani Iramba kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Stendi ya mabasi alisema wapuuze maneno yanayosemwa kwa lengo la kutaka kuwapotosha na kuwadanganya watu. 

Mlata alisema wananchi waendelee  kumuombea na kumuamini Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambae amejitoa kuwaletea maendeleo katika sekta ya maji, afya,umeme, barabara na elimu. 

Alisema adha ya usafiri waliyokuwa wakiipata wananchi huko nyuma, ambapo walilazimika kutoka Iramba kwenda kupanda gari Singida mjini kuelekea Dar es Salaam, lakini leo hii mabasi yanaanzia safari mjini Kiomboi kwa sababu ya uwepo wa barabara nzuri za lami. 

Mlata alisema wanafunzi walilazimika kutumia vibatari wakati wa kujisomea ambavyo viliingiza moshi puani hali ambayo hivi sasa haipo kwa sababu Rais Dk. Samia amefikisha umeme katika vijiji vyote, hivyo wanakila sababu ya kuendelea kumuunga mkono. 

Kuhusu elimu ameeleza watu walikua wanafaulu lakini anayepata bahati ya kuendelea na masomo anachaguliwa mmoja tu lakini hivi sasa shule zimejengwa katika kila kata kwa kutumia zana za kisasa. 

Akizungumzia kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, alisema ni tunu ya Taifa, wazee wao waliungana kwa sababu walikua wanataka kuleta maendeleo.

"Viongozi wangu wa  dini niwaombe muendelee kumuombea Rais wetu na kumtaka anayejiita mchungaji anayetamka kuwa Rais amekataliwa na Mungu akatubie kwa kuwa yeye ndio amekataliwa na Mungu kwa kukosa weledi wa kuhutubia," alisema. 

Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Lucy Boniface, alisema haikubaliki kwa kiongozi wa chama cha sisasa kuomba kibali cha kuhamasisha na kuimarisha chama chake halafu akiishapanda katika jukwaa anahubiri habari ya kuvunja Muungano. 

Alisema Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema atakae anza kusema sisi watanganyika na wao wazanzibari laana itamtafuna ndio maana chama cha kiongozi huyo kinatafunwa kwa sababu ya kutaka kuwarudisha Watanzania kwenye ukabila na ubaguzi wa kidini.