Hati za viwanja zatolewa saa 24 wizarani

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 10:54 AM Oct 26 2024
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi  Antony Sanga.
Picha: Mtandao
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Antony Sanga.

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imeanza kufanya kazi usiku na mchana kutatua migogoro ya ardhi na kutoa hati za viwanja.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi  Antony Sanga, alisema juzi wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ambaye yuko kwenye ziara za usiku kukagua miradi.

Sanga alisema utaratibu wa kufanya kazi usiku na mchana umekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa wamefanikiwa kutatua migogoro mingi na kwa muda huo wametoa hati 7,510.

Alisema walibaini kuwa wakati wa mchana kunakuwa na mrundikano wa watu wanaofika wizarani kupata huduma mbalimbali hali ambayo iliwalazimu kuanza kufanya kazi nyakati za usiku.

“Kuna watu hawana muda wa kuja mchana kwa hiyo usiku inakuwa nafasi yao kupata huduma na huduma hii si kwamba inapatikana hapa wizarani tu bali hata kwenye Manispaa za Kinondoni, Temeke, Jiji la Dasr es Salaam (Ilala), Ubungo  na Temeke wote wanatoa huduma za usiku,” alisema.

Alisema baadhi ya wafanyakazi wa wizara hiyo wamekuwa wakiingia kazini kuanzia saa 9:00 mchana na kumaliza kazi saa sita usiku baada ya kuonana na kusikiliza changamoto za wananchi.

Alhaji Ali Momba, ambaye alipata hati juzi usiku wizarani hapo, alisema baada ya kusikia huduma hizo zinapatikana usiku aliona ni bora aendelee na shughuli zake  mchana ili aje usiku na alikiri kuwa ni kweli alipokelewa na kupata huduma ndani ya muda mfupi.

“Utaratibu huu usiwe wa mpito, uwe wa kudumu ila waongeze mashine za kutolea huduma ila naishukuru wizara kwa ubunifu huu kwa sababu unaondoa usumbufu wa watu kukaa hapa muda mrefu, kuna wakati mtu anakaa hapa siku nzima,” alisema.

Mwingine aliyepewa hati ya ardhi usiku, Rehema Buguni, alisema huduma ya usiku imekuwa na manufaaa makubwa kwani wakati wa mchana kunakuwa na idadi kubwa ya watu na wanatumia muda mwingi sana kufuatilia masuala ya ardhi.

 Akizungumza kwenye tukio hilo, Chalamila alisema anashukuru kuona Mkoa wa Dar es Salaam umepewa makamishna wa ardhi wawili kutokana na ukubwa wa mkoa huo.

Alimshukuru Mhandisi Sanga kwa ubunifu huo ambao alisema utaondoa usumbufu wa foleni kwa wananchi wengi wanaokuja kutafuta suluhu ya matatizo ya migogoro ya ardhi.

Alisema wananchi wengi wanasumbuka sana na migogoro ya ardhi kutokana na tabia ya baadhi ya watu kughushi hati za viwanja na mashamba na kuviuza hali ambayo imesababisha mitafaruku.

“Nakushukuru sana Katibu Mkuu kwa sababu mmekuwa wasikivu sana mmetatua migogoro mingi sana ya ardhi na wananchi hapa wametoa mapendekezo kwamba  mashine za kutolea hati ni chache kwa hiyo wizara itafute namna ya kuziongeza ili kuhudumia wananchi kwa haraka zaidi,” alisema.

Chalamila alisema Mkoa wa Dar es Salaam umeweka azma ya kuhakikisha biashara zote zinafanyika kwa saa 24 hivyo kuanza kwa huduma hiyo ya usiku ni kuunga mkono azma hiyo.