MWILI wa aliyekuwa Mtangazaji wa kipindi cha Jahazi cha Kituo cha Radio cha Clouds FM, Gardner Habash, unatarajiwa kuagwa leo jijini Dar es Salaam na baadaye kusafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro kwa maziko.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na uongozi wa Clouds Media Group, maziko yanatarajiwa kufanyika kijijini kwao Kikelelwa, Kata ya Tarakea, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro kesho.
Ratiba hiyo ilionyesha kuwa, mwili wa Gardner ulipelekwa jana jioni nyumbani kwake Kijitonyama ambako kulifanyika ibada ya faraja kwa familia.
Kadhalika, leo saa mbili asubuhi, mwili utapelekwa kwenye viwanja vya Leaders Club vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam kwa ajili ya umma kupata nafasi ya kuaga.
Gardner alifariki juzi Aprili 20, mwaka huu alfajiri katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Gardner ambaye ni baba mzazi wa msanii wa Bongofleva, Malkia Karen, anakuwa ni Mtangazaji wa pili kufariki dunia akiwa anakitumikia kipindi hicho cha Jahazi cha Clouds FM, baada ya Ephraim Kibonde, aliyefariki dunia Aprili mwaka 2021, wakati anatibiwa katika Hospitali ya Bugando, jijini Mwanza.
Sehemu nyingine ambako Gardner aliwahi kufanya kazi ni Times FM, kupitia kipindi cha Masikani, pamoja na EFM ambako alianzisha kipindi cha Ubaoni kabla ya kurejesa tena Clouds FM, mwaka 2016.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED