DC Mhita afariji familia watoto kufa maji

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 03:54 PM Feb 18 2025
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita
Picha: Shaban Njia
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita

MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, amezifariji familia mbili zilizopoteza watoto wanne, wakati wakiogelea kwenye bwawa lililokuwa likitumika katika ujenzi.

Tukio hilo limetokea Februari 15, mwaka huu, majira ya jioni, wakati watoto hao wakitoka shambani kata ya Bulige, Halmashauri ya Msalala na kupita kwenye bawawa hilo kuogelea, na maji kuwazidi nguvu na kuzama.

Mhita amesema, maeneo yote yenye madimbwi au visima vya maji viwekewe uzio na mlango wa kuingilia na kutokea, ili kuwazuia watoto kuingia ovyo.

Aidha amewataka, TARURA na TANROAD, wanapomaliza ujenzi wa barabara, kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali za vijiji na kata juu ya mashimo waliyoacha wakati wakichimba molamu, ili waangalie namna ya kudhibiti lisileta maafa.

Bwawa la maji lililoua watoto wanne na mama yao katika kijiji na kata ya Bulige halmashauri ya Msalala
Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama, Stanley Luhwago, amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na walipopata taarifa walifika kwenye eneo la tukio haraka na kukuta tayari wananchi wameshawaopoa.

Amewataja kwa majina walikufa kuwa ni pamoja na Zawadi Nkwambi (13), Khadija Nkwambi (11), Rahel Peter (11), Samike Peter (01) pamoja na mama mzazi wa Samike, Hoja Kubo (29) aliyefariki wakati akijaribu kuwaokoa watoto hao.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, akipokea maelezo kuhusu bwawa lililosababisha vifo vya hivyo
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bulige, Allen Mahanga, amesema, ilikuwa ngumu kuopoa miili hiyo kwa sababu shimo hilo lilikuwa limejaa maji na kulazimika kutumia pampu kuvuta maji na miili iliyokuwa imenasa chini zaidi.

Mtendaji wa Kata hiyo, Emmanuel Mhina, amesema bwawa hilo lilikuwa sehemu mbaya na ilikuwa ngumu wao kuliona na waligundua wananchi wakilitumia kuchota maji ya kufua na kuogea na iliwafanya watoto kuingia na kuogelea.