DC Kolombo aagiza usafiri wa Meli kutoka Nyamisati kuelekea Mafia kurejea

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 07:07 PM Sep 11 2024

MKUU wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo
Picha: Julieth Mkireri
MKUU wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo

MKUU wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo ametoa siku mbili kwa Mamlaka ya Bandari na TEMESA kumpelekea taarifa ya kujieleza kuhusu chanzo kilichosababisha usafiri wa meli kutoka Bandari ya Nyamisati kwenda Mafia kukwama kwa siku nzima.

Kanali Kolombo ametoa maagizo hayo alipotembelea bandari hiyo na kungumza na abiria waliokwama katika bandari hiyo ambao walikuwa wakielekea Mafia.

"Ninawapa siku mbili ifikapo Septemba 12 nahitaji kupokea taarifa ya kunieleza nijue chanzo cha Changamoto hii ya kuendelea na safari," amesema.

Akiwa katika jengo la kupumzikia abiria katika Kijiji cha Nyamisati Kanali Kolombo amewakumbusha Mamlaka ya Bandari na TEMESA kuwa na tabia ya kutoa taarifa mapema wanapoona kuna viashiria vya kutokea kwa changamoto.

1

Kanali Kolombo ametoa pole na kuomba radhi kwa Wananchi waliokwama bandarini hapo na kuwahakikishia kuwa tayari amekwisha wasiliana na TEMESA na usafiri utarejea kama kawaida ambapo safari yao ilitarajiwa kuanza saa 8 usiku kulingana na ratiba ya maji kwa sasa lakini pia kutokana na kuharibika kwa tishari kisiwani mafia.

Akitoa ufafanuzi wa  mabadiliko ya safari hiyo Nahodha wa meli George Charles amesema moja ya sababu za usumbufu uliotokea ni kutokana na kuharibika kwa tishari (sehemu ya kushukua abiria)  katika mji wa mafia.

Hali hiyo inalazimu kwasasa meli kutia nanga ufukweni mwa bahari hivyo wanajitahidi safari zao zote zitazingatia ratiba ya kupwa na kujaa kwa maji katika kisiwani mafia.

Aidha wananchi waliokwama katika bandari hiyo wamemshukuru Kolombo kwa kusikia kilio chao na kufika kuwaona huku wakisisitiza umakini wa usimamizi wa bandari kuimarishwa zaidi ili kero hiyo isijirudie tena.
2