CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza kuanza tena maandamano ya amani ngazi ya mikoa, safari hii ikianza na Moshi Mjini mwishoni mwa Aprili mwaka huu.
Maandamano hayo yanalenga kuendelea kuishinikiza serikali kuja na mpango wa dharura wa kukwamua makali ya maisha wanayopitia Watanzania kwa sasa.
Jana, Mwenyekiti wa CHADEMA, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, alisema maandamano hayo yatawahusisha viongozi wa kitaifa, akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe.
“Moshi tunakuja kwenye maandamano mwisho wa mwezi wa nne, mimi nitakuja kwenye maandamano hayo. Mwenyekiti Mbowe na yeye atakuja kuandamana Moshi.
“Tutakapotangaza tunaomba njooni barabarani. Huu ni mji unaowakilishwa na wajanja, hatuwezi kuwa na wajanja halafu hatuwezi kuja kwenye maandamano.” Alisema Lema.
Katika mkutano huo, pamoja na mambo mengine Lema alisema mabadiliko ya tabianchi yanayoitikisa dunia kwa sasa yanakwenda kusababisha nchi nyingi za Afrika kuwa na njaa.
“Hali inaenda kuwa mbaya sana kwa sababu ya namna tunavyojipanga kuhimili mabadiliko hayo. Tunahitaji viongozi ambao wana maono ya kuacha kusubiri kesho na kuyamaliza leo,” alisisitiza.
Katika mkutano wa kuhitimisha ngwe ya pili ya maandamano ya majiji uliofanyika Februari 26 mwaka huu, Mbowe alisema katika majiji yote waliyofanya maandamano walitembea kilomita 166.
Mbowe aliyataja majiji hayo kuwa ni Mbeya, Mwanza, Dar es Salaam na Arusha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED