CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kitaweka mawakala katika vituo vinavyoandikisha wananchi katika daftari la wakazi nchi nzima ili kuhakikisha kuwa wapiga kura wasio halali hawaingizwi katika madaftari hayo ili kudhibiti wizi wa kura wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kauli hiyo imekuja ikiwa zimebaki siku tatu uandikishaji wananchi katika daftari hilo uanze ambapo unatarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 11 hadi 20, mwaka huu.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, amewaeleza waandishi wa habari leo, Jijini Dar es Salaam kuwa mawakala wao wataweka kambi katika vituo hivyo kwa siku 10 ili kuhakikisha kuwa wananchi halali wa eneo husika ndio wanaoandikishwa katika daftari hilo.
“Tukifanikiwa kulinda haki, ukweli, uhuru, demokrasia , maendeleo kupitia uandikishaji wa wapigakura safari itakuwa rahisi sana kwenye hatua nyingine zinazofuata.” amesema
Ametoa rai kwa Watanzania wowote kutoa msaada wa hali na mali kama vile maji ya kunywa kwa mawakala wa chama hicho wataojitolea kusimamia uandikishaji huo kwa siku 10 ili haki itendeke.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED