KATIBU wa Oganaizesheni wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Omar Ibrahim Kilupi, amekemea tabia ya baadhi ya wanasiasa waohamasisha udini, ukanda na ukabila.
Kutokana na kuwapo kwa wanasiasa hao, amewataka viongozi wa dini na wananchi kukemea tabia hizo .
Alisema hayo juzi wakati akizungumza na waumini wa dini ya Kikiristo katika hafla ya kutimiza miaka 30 ya Kwaya ya Mtakatifu Michael Malaika Mkuu, Parokia ya Mpendae, Zanzibar.
Kilupi alisema viongozi wa dini nchini wanatakiwa kuelekeza nguvu zao katika kuhubiri na kutoa mafundisho ya kiimani ya kukemea kauli za uchochezi na ukabila zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa kwa kuwa zinaweza kuingiza nchi katika machafuko.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, wameasisi maridhiano ya kisiasa na kuruhusu utawala wa demokrasia, hivyo ni muhimu kwa kila mwananchi kuheshimu misingi hiyo.
Pamoja na maridhiano hayo, alisema kuna baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wameanza kutoa kauli zinazoashiria uvunjifu wa sheria, ambazo zinazotakiwa kupingwa na wananchi wote bila kujali tofauti zao za kisiasa na kidini.
Kilupi aliwasihi viongozi na waumini hao kuendeleza umoja, mshikamano na upendo wakati wote sambamba na kuiombea nchi iendelee kuwa na amani na utulivu.
“Wito wangu kwenu endeleeni kuwa wamoja. Msikubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa wanaohamasisha vurugu na kauli za kuwabeza viongozi wetu wakuu wa kitaifa kwani maendeleo yanayotekelezwa nyote mnayaona.
“Amani ndilo chimbuko la maendeleo haya tuliokuwa nayo hivi sasa hivyo tusikubali fursa hii ituponyoke kwa gharama yoyote,” alisema Kilupi.
Kilupi alisema CCM imeendelea kusimamia sera zake kwa kuhakikisha serikali inatekeleza kikamilifu maendeleo kama ilivyoahidi katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.
Pia aliwasisitiza waumini hao kutumia vizuri haki yao ya kidemokrasia kuhakikisha wanajiandikisha katika awamu ya pili ya daftari la kudumu la wapigakura ili wapate uhalali wa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Naye Padri Antony Kanturu wa Parokia ya Mpendae, alisema kipaumbele cha kanisa hilo ni kutoa mahubiri yanayowaunganisha wananchi katika kuendeleza amani na upendo.
Katika risala yao, wanakwaya walisema kwa kipindi cha miaka 30 wamepata mafanikio mbalimbali yakiwamo kurekodi na kutengeneza albamu za nyimbo mbalimbali zinazoendelea kufanya vizuri katika soko la nyimbo za injili ndani na nje ya nchi.
Aidha walitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni ukosefu wa gari ya kutoa huduma za usafiri na ukosefu wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya uandaaji wa nyimbo.
Kwaya hiyo ya Mtakatifu Michael Malaika Mkuu, ilianzishwa mwaka 1994 ikiwa na wanakwaya 15.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED