ASKARI wawili wa Hifadhi ya Taifa ya Wanyamapori ya Katavi, wanashikiliwa na polisi mkoani Katavi kwa tuhuma za kumuua kwa kumpiga risasi kijana mmoja wa jamii ya kifugaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kamishna msaidizi Mwandamizi (SACP) Kaster Ngonyani, alithibitisha kukamatwa kwa askari hao wanaodaiwa kufanya mauaji hayo Desemba Mosi, mwaka huu, katika kijiji cha Ikuba, Halmashauri ya Mpimbwe, wilayani Mlele.
Kijana aliyeuawa ni Ngimbangu Mandalu (25) ambaye anadaiwa kupigwa risasi na askari hao akiwa katika harakati za kuwakimbia pindi walipotaka kumkamata kwa madai ya kuingiza mifugo katika eneo lililohifadhiwa na kijiji ambalo shughuli za kibinadamu hiziruhusiwi kufanyika.
Baba mkubwa wa marehemu, Maduka Salawa, alisema siku ya tukio aliarifiwa kuwa mtoto wake amepigwa risasi, hivyo aliongozana na viongozi wa kata, akiwamo polisi na kufika eneo husika.
Alisema baada ya kufika ilibainika kwamba kijana huyo aliuawa akiwa nje ya mipaka ya maeneo hayo yanalindwa na askari wa TANAPA.
Salawa alisema baada ya askari hao kumpiga risasi kijana huyo, waliichukua maiti yake na kwenda kuitupa porini, lakini kutokana na ndugu wa marehemu kulalamika kwa viongozi wa juu wa wilaya na wa hifadhi, ndipo watuhumiwa walionesha maiti hiyo.
Kutokana na mazingira hayo, alisema ndugu wa marehemu waliamua kutochukua mwili huo hadi kupata tamko la serikali kuhusu mauaji hayo.
Alisema maiti hiyo ilikaa hospitalini kwa siku tatu ndipo jana walipoichukua na kwenda kuzika, baada ya kujiridhisha kwamba watuhumiwa wamekamatwa.
January Joseph, shuhuda wa tukio hilo, alidai watuhumiwa walimkimbiza Mandalu na baada ya kuona anawazidi mbio, walifyatua risasi na kumjeruhi mguuni upande wa goti, kifuani na begani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED