Aliyekuwa RC Simiyu akamatwa tuhuma za kulawiti mwanachuo

By Rose Jacob , Nipashe
Published at 09:38 AM Jun 14 2024
liyekuwa Mkuu wa Mkoa  wa  Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda (46).
Picha: Maktaba
liyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda (46).

JESHI la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda (46), kwa tuhuma za kulawiti binti mwenye umri wa miaka (21).

Inadaiwa Dk. Nawanda mnamo Juni 2, mwaka huu, majira ya usiku, katika eneo la baa ya The CASK iliyoko viwanja vya jengo la Rock City Mall, jijini Mwanza, alilawiti binti huyo, mwanafunzi wa chuo cha mkoani Mwanza. 

Akithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilboard Mutafungwa, alisema walimkamata jana saa sita mchana.

"Mtuhumiwa tumemkamatia jijini Mwanza kwa tuhuma kumwingilia kinyume cha maumbile binti ambaye jina limehifadhiwa, katika eneo la maegesho ya magari ya baa ya The CASK.

"Mahojiano yanaendelea kwa kushirikisha taasisi zingine. Yakikamilika yatapelekwa Ofisi ya Mashtaka ya Taifa kwa ajili ya kulisoma jalada hilo ili kuandaa mashtaka dhidi ya mtuhumiwa," alisema.

Kamanda Mutafungwa alifafanua kuwa katika kushughulikia suala hilo, mtuhumiwa huyo atashtakiwa na Jamhuri na mlalamikaji ni shahidi katika kesi hiyo, huku akikanusha nyaraka zinazosambaa mitandaoni kuhusiana na suala hilo kwamba si sehemu ya uchunguzi wao.

Alisema gari linalodaiwa kutumika katika ukatili unaodaiwa kutendwa na Dk. Nawanda nalo linashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Simiyu litapelekwa Mwanza.

Alionya wanaosamabaza taarifa kuhusiana na tukio hilo bila kujali utu wa binti huyo, watambue wako kinyume cha sheria ya kulinda utu wa mtu.

Kwa mujibu Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, Kifungu cha 154(1), mtu anayepatikana na hatia ya kulawiti, adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 gerezani au kifungo cha maisha kama ametenda kitendo hicho kwa mtu mwenye umri wa chini ya miaka 10.