ACT Wazalendo yalia maoni yao kukaliwa

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 11:11 AM Apr 29 2024
Kiongozi mpya wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu.
PICHA: MAKTABA
Kiongozi mpya wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu.

MKUTANO Mkuu wa Kidemokrasia wa Chama cha ACT Wazalendo, umeibua hoja ikiwamo madai kuwa kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia Zanzibar yamekaliwa, hayajafanyiwa kazi, huku hoja kuhusu Zanzibar yenye mamlaka kamili ikitawala.

Aidha, madai ya kuwapo viashiria hali ya nchi kiuchumi kutokuwa nzuri.

Kiongozi mpya wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, akizungumza katika maadhimisho ya miaka 10 ya kuzaliwa chama hicho na mkutano wa kidemokrasia uliofanyika Moshi, Kilimanjaro, amesema miaka 10 ya ACT Wazalendo imekuwa ikipitia kwenye pumzi ya moto.

Amelisema kwa sasa mabega yake ni mazito na chama chake kinaona sera zinazotekelezwa na Serikali ya CCM hazijali maslahi ya wengi, badala yake viongozi wa kisiasa na umma wanatumia mwanya kujiimarisha katika maslahi binafsi dhidi ya umma na kuzima ndoto za ujenzi wa taifa la watu wote.

Aidha, Chama hicho kimetangaza rasmi Mei 5, mwaka huu, kuanza kutumia nembo yake mpya na bendera mpya, kujipanga kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025.

“Pamoja na kwamba nchi yetu imejaliwa rasilimali nyingi, raia wake kwa umoja wao hawafaidiki na rasilimali, lakini zinaendelea kuwaneemesha watu wachache walio serikalini, mashirika ya umma na kampuni za kimataifa.

“Bado, uchumi wa taifa huru unaendelea kuwatajirisha watu wa nje na wachache wa ndani ya nchi, huku mamilioni ya Watanzania wakifukarishwa.”

Semu, ameeleza kuwa Watanzania wanaweza kuona viashiria kadhaa vya hali ya nchi yao kiuchumi sio nzuri na haielekei pazuri, akieleza kasi kubwa ya ukuaji wa deni la serikali, kutishia maendeleo ya watu, uwezo wa nchi kujihudumia na kusababisha ukuaji wa uchumi unaoendeshwa na deni (debt driven growth).

Suala la huduma za afya na kupaa kwa gharama za matibabu, kukosekana kwa huduma bora au kutokuwapo kwa miundombinu itakayowaweza wananchi kuyapata.

Aidha, akizungumzia ukosefu wa ajira na kipato cha uhakika, amesema kuwa takwimu zinaonyesha vijana milioni moja wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka, ni 67,000 pekee wanaoweza kuajiriwa.

“Kwa hiyo, nguvu kazi kubwa iliyotupwa nje ya mfumo wa uzalishaji inatumika kuwanufaisha watu wachache kwa kuzalisha faida zaidi, huku wakiwafukarisha na kuwadunisha mamilioni ya Watanzania, alieleza katika hotuba yake.

Kwa ufupi, hoja nyingi zinazotolewa hazidadisi kiini cha tatizo la ukosefu wa ajira nchini kwetu.”

Kuhusu kikokotoo cha mafao kwa wastaafu alisema, matumizi ya kanuni mpya za kikokotoo kwa kumlipa mstaafu asilimia 33 ya mafao ya mkupuo kwa miaka 12.5 na kikotoo cha 1/580 ni kuwakandamiza na kuwanyonya wazee waliotumikia taifa katika mazingira magumu ya mishahara ya chini inayowafanya kuishi kwenye mzunguko wa madeni.

Semu,  amesema kanuni hizo zinashusha ari, hamasa na ufanisi wa kazi kwa wafanyakazi.

Kuhusu hali ngumu ya maisha na umaskini, alisema kwa picha ya jumla, hali ya kiuchumi inawaonyesha kuwa bado mapambano yao ya kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika na zinalinufaisha taifa (kwa maslahi ya wote na sio wachache wale wale), yanapaswa kuendelea na kuongezewa nguvu.

Makamu Mwenyekiti Bara na Waziri Mkuu Kivuli wa chama hicho, Isihaka Mchinjita, wakati wa mjadala wa mwenendo wa demokrasia nchini kuelekea chaguzi zijazo,  amesema chama hicho hakiko tayari kushuhudia hujuma za uchaguzi na waliowahujumu waje mbele yao wameinamisha shingo.

Kuhusu Sheria za Uchaguzi na Tume Huru ya Uchaguzi, Mchinjita,  amesema hawana tatizo la maoni yaliyotolewa na Kikosi Kazi cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwa yapo na yamewekwa hadharani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Samia Suluhu Hassan).

Hata hivyo,  amesema shida yao ni maoni ya Kikosi Kazi cha Zanzibar, kushikiliwa bila kufanyiwa kazi.

Zitto: Natamani ningefanya biashara

Mwasisi na Kiongozi wa zamani wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akichagiza mjadala kuhusu mwanzo mpya wa chama hicho, operesheni ya shusha tanga alisema:

“Nadhani jambo ambalo ningepaswa kulifanya kama maisha yangu yangerudi tena nyuma miaka 20 ni kufanya biashara. Mimi nilikuwa siamini kabisa kwamba ukiwa kiongozi hupaswi kufanya biashara, nilikuwa naamini hivyo hata kuuza maandazi; kwa sababu utafanya maamuzi yenye mgongano wa maslahi na imekuwa hivyo muda mrefu.

“Lakini mara baada ya kuwa kiongozi wa ACT Wazalendo, sasa moja kati ya kazi ya viongozi wa chama yeyote duniani kote; kazi yake ya kwanza ni fund raising between 65 and 75 percent (kutafuta fedha kati ya asilimia 65 mpaka 75) ya muda wa viongozi wa chama. Kwa hiyo mkimsikia Doroth (Semu) anasema mabega mazito ni kwa sababu hiyo.

Miaka 10 ya uongozi wangu, nimejifunza nilikosea sana kuacha kufanya biashara. Kwa sababu katika kazi za chama mfano shughuli kama hii inahitaji gharama za usafiri, wafanye nini, halafu chama hakizalishi, pesa za chama unaziomba kwa watu.

 Unaishi kwa kugongea wafanyabiashara. Anajua tu huna, lakini anakwambia atakupa halafu mpaka kesho shughuli anakuambia mambo yangu yameenda vibaya bwana!