Wenye ulemavu hati hati kupata mikopo

By Oscar Assenga , Nipashe
Published at 08:33 AM Jan 24 2025
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian.
Picha: Mtandao
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian.

JAMII ya watu wenye ulemavu katika halmashauri 11 za Mkoa wa Tanga hazijajengewa uwezo wa kutosha kushawishika kupata mikopo ya asilimia 10 kupitia makusanyo ya ndani, imegundulika.

Kutokana na hali hiyo,  Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, ameagiza maofisa maendeleo ya jamii wa halmashauri hizo kushirikiana na wadau, ikiwemo Chama cha Watu Wenye Ulemavu Tanzania (CHAWATA) kutoa elimu kuhusu mikopo hiyo ili kundi hilo likikidhi vigezo vya kunufaika na fursa hiyo. 

 Dk. Batilda alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza  na Nipashe baada ya kuzindua  dirisha la mikopo hiyo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu mkoani hapa  baada ya  kugundua hilo.

“Mkoa wa Tanga, kuna jumla ya shilingi bilioni tisa zimetengwa kwenye halmashauri zetu zote kukuza biashara, uchumi, maendeleo na ustawi wa wanufaika na jamii kwa ujumla.

 Lakini wenye ulemavu bado wako nyuma. Hawana elimu ya kutosha kuhusu mikopo hii ndio maana natamani wapate elimu bora na msaada wa karibu kuwasaidia kuwa na fursa ya kujiendeleza kiuchumi,” alisema.

1

 Julai mosi mwaka jana, serikali ilirejesha fedha za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri  nchini baada ya kusitishwa Bungeni, Dodoma Aprili 13, mwaka juzi. 

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, Halmashauri za Kilindi, Korogwe Mji, Lushoto, Mkinga, Pangani na Tanga Jiji, zimetoa mikopo kwa walengwa wa mpango huo.

 Halmashauri za Handeni, Korogwe, Bumbuli, Muheza na Handeni Mji, ziko katika hatua za mwisho  kuchakata maombi ya vikundi kwa mujibu wa taratibu kwa ajili ya kupata mikopo hiyo kwa ajili ya ujasiriamali.