Wastaafu polisi wadai bilioni 97/-

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 11:02 AM Jan 29 2025
Naibu Waziri Daniel Sillo.
Picha: Mtandao
Naibu Waziri Daniel Sillo.

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema askari polisi wastaafu wanadai kiasi cha Sh. bilioni 97.12 na kwamba serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kulipa madai hayo.

Naibu Waziri Daniel Sillo aliyasema hayo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Maida Hamad Abdallah. Mbunge huyo alitaka kujua lini serikali itawalipa madai ya muda mrefu askari polisi waliomaliza muda wao wa utumishi.

Akijibu swali hilo, Sillo alisema serikali inaendelea kulipa madai ya askari polisi waliomaliza muda wao wa kazi baada ya kustaafu wanadai Sh. 97,120,011,700.26.

Alisema mpaka sasa madai yaliyohakikiwa na kuwasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo ni Sh. 75,214,744,005.10.

“Kwa sasa madai yanayoendelea kuhakikiwa ni ya mwaka wa fedha 2023/24 na Sh. 21,905,267,695.16 zinadaiwa. Pindi  uhakiki ukikamilika, madai yote yatawasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo,” alisema.

Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Asha Abdallah Juma, alihoji kwa nini mifumo ya kielektroniki isitumike kuweka taarifa zote muhimu za askari ili atakapofika umri wa kustaafu, asisotee malipo.

“Kumekuwa na mlolongo mkitaka athibitishe aliajiriwa lini, alipandishwa cheo lini na alikopa kitu gani huu ni usumbufu. Pia serikali inatambua kuwa askari hao kwa sasa wanahitaji hayo mafao kushinda siku nyingine yoyote,” alisema.

Akijibu swali hilo, Sillo alisema serikali imeendelea kufanya kazi kubwa ya mifumo ya kielektroniki kuhakikisha taarifa zote za askari zinaingia kwenye mfumo, ili kuepusha usumbufu wanapomaliza muda wao wa utumishi ili walipwe kwa wakati.