UTENGENEZAJI wa bidhaa zisizokuwa na ubora unaohitaji katika soko la ndani na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unasababisha wajasiriamali wengi nchini kukosa nembo ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), imeelezwa.
Hayo yalielezwa jana na wajasiriamali wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga katika mafunzo ya uzalishaji, usindikaji na ufungashaji wa bidhaa za uokaji yaliyotolewa na TBS Kanda ya Ziwa.
Mmoja wa wajasiriamali hao, Shamu Saidi alisema kuwa utengenezaji wa bidhaa zisizo kuwa na ubora ni chanzo cha kuendelea kukosa nembo ya TBS na kubaki na soko la ndani ambalo ushindani wake ni mkubwa.
Shamu aliiomba TBS kuendelea kuwapatia elimu endelevu ya namna sahihi ya utengenezaji na ufushangashaji wa bidhaa wanazozalisha na kupata nembo ya shirika hilo baada ya kukaguliwa na wataalamu wa shirika hilo.
" Bidhaa nyingi tunazalisha majumbani mwetu hasa mikate na zile za usindikaji ambako mazingira yake sio rafiki kwani kuna mwingiliano mkubwa wa wanafamilia na majirani ndiyo sababu tunapozipeleka ofisi za TBS kuangalia viwango na kupata nembo, lakini zinakutwa hazina sifa na kutupwa," alisema.
Aaliiomba Ofisi ya Mkuu wa Wilaya iwapatie maeneo ya wazi pembezoni mwa barabara kwa kuwa yana mandhari nzuei ya maua na miti ili wajenge viwanda vidogo vya kuoka mikate na kusindika bidhaa hali ambayo itasaidia kutangaza bidhaa na kupata masoko ya uhakika.
Abdullah Juma, alisema elimu watakayoipata itawawezesha kujenga imani kwa wateja wao bidhaa wanazozalisha ni salama kwa matumizi ya binadamu kwa kuwa zitakuwa na nembo ya ubora ya TBS.
Meneja wa Mafunzo na Utafiti wa TBS wa kanda hiyo, Hamisi Sudi alisema kuwa wafanyabiashara na wajasariamali wanazalisha bidhaa nyingi ambazo hazina viwango na ubora unaohitajika na kushindwa kukabiliana na ushindani katika soko la ndani na EAC.
Sudi, alisema elimu wanayotarajia kuitoa kwa wajasirimali hao ni pamoja kufahamu mahitaji ya soko la EAC, viwango vya ubora wa bidhaa wanazozalisha na faida.
Alitaja nyingine ni kupata elimu ya matakwa ya viwango vya bidhaa za uokaji, usajili wa biashara, kanuni bora za usindikaji na utaratibu wa uthibitisho wa ubora wa bidhaa.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita aliitaka TBS kuongeza wigo wa kuwafikia na kuwaelimisha wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo ili kuwa na bidhaa bora ambazo zitalinda afya mtumiaji wa mwisho na kukabiliana na ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED