WADAU wa maendeleo, wameanza ‘kumwaga’ fedha zitakazosaidia kutekeleza mpango wa ‘mission 300’ wa kufikisha umeme kwa watu milioni 300 katika bara la Afrika.
Walitoa ahadi ya kuanza kutoa fedha hizo wakati wakizungumza mbele ya marais walioshiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, uliomalizika jana, jijini Dar es Salaam.
Wadau hao ni Benki ya Maendeleo ya Afrika(AFDB), Benki ya Dunia (WB), Benki ya Kiislam, Shirika la Maendeleo ya Miundobinu na Mfumo wa Kimataifa unounganisha nchi zinazouza mafuta (OPEC).
Rais wa AFDB, Dk. Akinwumi Adesina na WB, alisema wametenga Dola za Marekani bilioni 40 kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa mpango wa awali wa mpango huo wa Mission 300 wa kufikisha nishati ya umeme kwa wananchi milioni 300 katika nchi za Afrika.
Kati ya hizo, Dola bilioni 22 zitatolewa na WB na Dola bilioni 18.2 zitatolewa na AFDB.
Kadhalika, alisema Rais wa Benki ya Kiislamu ameahidi kutoa Dola bilioni 2.6, Rais wa Maendeleo ya Miundombinu akiahidi kutoa Dola bilioni 1.5 na Rais wa Mfuko wa OPEC akiahidi kutoa Dola bilioni moja.
Dk. Adesina, alisema upatikanaji wa umeme ni nyenzo muhimu kwa ukuaji wa uchumi na ukosefu wa nishati hiyo unapunguza ukuaji wa uchumi kwa asilimia 2.4.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Amina Mohamed, aliipongeza Tanzania kwa kupanua huduma ya upatikanaji wa nishati ya umeme, ikiwamo kuwekeza katika nishati mbadala na kwamba sio tu kutakuza ukuaji wa uchumi, lakini pia kutachochea upatikanaji wa ajira.
Alisema katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja, Tanzania imeongeza kasi ya upatikanaji wa umeme, kutoka asilimia 14 mwaka 2011 hadi 46 mwaka 2022.
Alisema nchini Tanzania, zaidi ya taasisi za kijamii 60,000 zikiwamo shule 12,905, vituo vya kutolea huduma za afya 6,768 na sehemu za kazi zaidi ya 8,000 zimeunganishwa na umeme wa uhakika.
Alisema mikakati ya nchi hiyo kuhamasisha nishati mbadala ni miongoni mwa kichocheo cha mabadiliko ya kiuchumi barani Afrika.
MIPANGO YA TANZANIA
Rais Samia Suluhu Hassan alisema Tanzania ni moja ya nchi 12 zinazotekeleza mpango mahsusi wa taifa kuhusu nishati ambao utaongeza kasi katika kuunganisha umeme nchini hadi kufikia asilimia 72 ifikapo mwaka 2030.
Alisema ili kufanikisha mpango huo ndani ya miaka mitano, inahitaji uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni tano zitakazopatikana kutoka katika sekta binafsi.
Pia, alisema kupitia mpango huo, Tanzania imejipanga kutekeleza mambo manne ikiwamo kuongeza uzalishaji wa umeme kutokana na nishati mchanganyiko kwamba mpaka sasa ina uwezo wa kuzalisha megawati 3,431 na asilimia 58 inatokana na vyanzo vya maji, 35 gesi asilia na saba kutoka vyanzo vingine.
Kadhalika, Tanzania imelenga kuongeza megawati 2,463 za nishati kutokana na jua, gesi asilia, upepo na vyanzo vingine ifikapo mwaka 2030.
Alisema mweleko wa Tanzania kwa sasa ni kufikisha vitongoji 64,359 na mpaka sasa imeshavifikia vitongoji 32,827.
Aidha, Tanzania ni kiungo muhimu katika kuunganisha nishati kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (SADC) na kuwezesha biashara ya umeme kutoka Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri.
Tayari Tanzania imeunganisha miundombinu ya umeme katika nchi za Burundi, Rwanda na Kenya na sasa inaendelea kuunganisha katika nchi ya Zambia na Uganda na kwamba uwapo wa miundombinu hiyo utawezesha biashara ya nishati katika nchi za Jumuiya ya Afrika na SADC.
Rais Samia alisema nchi yake imeweka mkakati wa taifa wa nishati safi kupikia unaolenga kupandisha kiwango cha matumizi ya nishati hiyo safi ya kupikia kutoka asilimia 10 hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2030 na mpango mahsusi uliozinduliwa jana utasaidia kufikia lengo hilo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED