UWANJA wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato mkoani Dodoma ambao utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa na abiria 1,500,000 kwa mwaka, unatarajiwa kuanza kutumika Oktoba mwakani.
Hayo yalisemwa juzi jijini Dodoma na Msimamizi wa mradi huo Mhandisi wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS, Mahona Luhende, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini walipotembelea mradi huo.
Alisema mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu Sh. bilioni 360 ambazo ni mkopo nafuu wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) wakati serikali ya Tanzania ilitoa fidia kwa wananchi waliokuwa wanaishi eneo hilo.
Alisema uwanja huo unajengwa na kampuni mbili za Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd inayojenga majengo ya uwanja huo na Kampuni ya Sinohydro Corporation Ltd inayojenga miundombinu ya barabara.
Alisema mkandarasi wa ujenzi wa majengo ya uwanja huo Beijing Construction alianza ujenzi huo Novemba mwaka 2022 na amefikia asilimia 22.5 na kwamba anatarajiwa kukamilisha ujenzi Oktoba mwaka 2025.
Alisema mkandarasi wa miundombinu ya barabara za uwanja huo amefikia asilimia 56 ya ujenzi.
“Mvua zilizonyesha zilisababisha baadhi ya shughuli kusimama na bila mvua huenda mkandarasi wa majengo ya uwanja angekuwa amefikisha asilimia 60 lakini tunafurahi kuona kwamba mkandarasi wa barabara za uwanja ameshafikia asilimia 56,” alisema.
Alisema sehemu ya kurukia na kutua ndege imefikia sehemu nzuri na kwamba wanatarajia mpaka Oktoba mwaka huu baadhi ya ndege zitaanza kupelekwa kutua kama sehemu ya majaribio.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED