JUMUIYA ya kimataifa, hususan mabalozi wa nchi mbalimbali walioko Tanzania, pamoja na Algeria, Uganda India na Marekani, wamepongeza uteuzi wa Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu, Oktoba, mwaka huu.
Mbali na kumpongeza Samia, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM na Rais, mabalozi hao pia, wamewapongeza Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Urais pamoja na Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuthibitishwa kuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar.
Mabalozi hao, wametoa pongezi hizo wakati wa mazungumzo yao na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Nchimbi, yaliyofanyika kwa nyakati tofauti leo katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi wa Algeria Nchini, Ahmed Djellal, ameangazia pia uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Algeria, hususan mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Afrika.
Balozi huyo ametoa pongezi kwa Rais Samia, Rais Dk. Mwinyi na Balozi Nchimbi, kwa kuaminiwa kupeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Balozi Nchimbi na Balozi Djellal pia, wamejadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na Algeria, kupitia sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu wa kiuongozi na fursa za masomo.
Katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi wa India nchini Tanzania, Bishwadip Dey, ameeleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na India, umeendelea kuimarika na kunufaisha pande zote mbili, hususan katika sekta za biashara, uwekezaji, teknolojia na afya.
Kadhalika, ametoa pongezi kwa CCM kwa kuwaamini Rais Samia, Rais Mwinyi na Balozi Nchimbi, kuwa wagombea wake katika uchaguzi huo.
Lentz pia ametoa pongezi zake na kuwatakia kila la heri Rais Samia, Rais Mwinyi na Balozi Nchimbi kutokana na uamuzi ya Mkutano Mkuu Maalum wa CCM.
Kwa upande wake, Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali Mstaafu Fred Mwesigye, amefikisha salamu za pongezi kutoka kwa Serikali ya Uganda na chama tawala cha NRM, akieleza kuwa Uganda inatambua na kuheshimu mchango wa Tanzania na CCM katika harakati za ukombozi wa Afrika.
Amemhakikishia Balozi Nchimbi kuwa uhusiano wa kidugu kati ya Tanzania na Uganda, utaendelea kuimarika kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Balozi Mwesigye amesisitiza kuwa urafiki wa kihistoria kati ya Tanzania na Uganda, umejengwa juu ya misingi imara ya mshikamano wa kikanda, ushirikiano wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi, ambao utaendelea kuimarika kwa ustawi wa mataifa hayo mawili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED