Usajili wa mtandaoni kupata mkopo wa asilimia 10 wawatoa jasho wajasiriamali

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 01:42 PM Apr 17 2024
Katibu jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi, Wilaya ya Ilala, Lucy Mbwale, akizungumza katika mkutano huo.
Picha: Sabato Kasika
Katibu jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi, Wilaya ya Ilala, Lucy Mbwale, akizungumza katika mkutano huo.

BAADHI ya wanawake wajasiriamali, wamedai huenda wakakosa mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na halmashauri, kwa maelezo kuwa mfumo mpya wa kujisajili mtandaoni bado ni kikwazo kwao.

Wamedai pia kwamba, pamoja na kutokuwa na uelewa wa jinsi ya kutumia simu janja kujisajili, vilevile, wengi wao hasa wa vijijini wana  simu za vitochi, ambazo haziwezi kutumika kujisajili mtandaoni.

Ni katika mkutano iliojadili fursa za mikopo ikiwamo inayotolewa na halmashauri, uliofanyika Kata ya Kipunguni Dar es Salaam jana, ukishirikisha wanawake wajasiriamali zaidi ya 80 kutoka kata hiyo.

Mkutano huo uliandaliwa na Kituo cha Jamii Kipunguni kwa kushirikiana na shirika la kuinuka Wanawake kiuchumi la Nyayo Tanzania, ili kujua kama wanaelewa utaratibu mpya kupata mikopo.

Adelina Mluge ambaye ni Mkurugenzi Shirika la Solidarity for Women and Children with Disabilities (SOWOCHIDI), amesema, huenda mikopo hiyo ikachukuliwa na wakubwa huku walengwa wakikosa.

"Tunaambiwa tujisajili mtandaoni, lakini wanawake wengi hawajui jinsi ya kutumia simu janja, lakini pia wenzetu wa vijijini hawana simu janja, hivyo ni vyema tuelimishwe zaidi jinsi ya kujisajili," amesema Adelimna.

Baadhi ya wanawake wajasiriamali wakiwa katika mkutano huo.
Mjasiriamali mwingine, Zaidan Kindamba, amesema yeye hajui lolote kuhusu utaratibu mpya wa kupata mikopo hiyo, na kwamba ilikuwa ni mara yake ya kwanza kusikia utaratibu mpya kwenye mkutano huo.

"NInadhani kuna haja ya kutuelimisha ili tuwe na uelewa wa kutosha, tujue jinsi ya kujisajili mtandaoni, vinginevyo inaweza kutuwia vigumu kupata mikopo hiyo," amesema Zaidan.

Katibu jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi, wilaya ya Ilala, Lucy Mbwale amewataka  waajasiriamali hao kutokata tamaa, badala yake waende kwa Ofisa Maendeleo ya Jamii wa kata hiyo awaelekeze jinsi ya kujisajili.

"Pamoja na umuhimu wa wa elimu kwa ajili ya kuuelewa mfumo huo, bado mna nafasi kwenda ofisa huyo anajua maelekezo yote ya kujisajili katika mfumo," amesema Lucy.

Baada ya kuonekana  kwamba, wajasiriamali wengi hawana uelewa kuhusu kujisajili mtandaoni, Mkurugenzi wa Kituo Cha Sauti ya Jamii Kipunguni, Seleman Bishagazi amesema kituo hicho kitashirikiana na shirika la Nyayo Tanzania kutoa elimu kwa waajasiriamali hao.

Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, imetenga Sh. bilioni 11 za mikopo ya asilimia kumi inayotolewa katika ngazi ya halmashauri ili kuwawezesha wajasiriamali wa wilaya ya Ilala, kukuza mitaji yao.

Mkuu wa wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo alisema hayo hivi karibuni, katika kongamano la wanawake wa jimbo la segerea la miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan.