MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejivunia mafanikio kutokana na sekta ya mawasiliano kukuza uchumi nchini kwa kuongeza usajili wa laini za simu nchini kwa asilimia 7.7 kwa robo ya mwaka jana.
Mafanikio hayo yalitangazwa na Mkurugenzi wake wa masuala ya kisekta , Mwesigwa Felician kwenye semina kwa wahariri, waandishi na watangazaji wa vyombo vya habari Mkoa wa Mwanza kuhusu taarifa za mwenendo wa sekta ya mawasiliano kwa robo hiyo ya kuanzia Oktoba hadi Disemba mwaka jana.
Felician, alisema kwa kipindi hicho mamlaka hiyo iliongeza laini hizo kutoka milioni 80.7 za Oktoba hadi millioni 86.8 Disemba mwaka jana na kuwa hatua hiyo ni mafanikio kiuchumi kwa taifa.
Alisema ongezeko la idadi ya laini za simu zinazotumika nchini ni fursa na hatua muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia sekta ya mawasiliano.
Alisema ongezeko hilo pia ni kwa watumiaji wa huduma ya inteneti kutoka milioni 40 hadi milioni 48 huku watumiaji wa simu janja wakifikia milioni 23.
Vilevile, alisema idadi ya dakika nchini imeongezeka hadi kufikia bilioni 42.5 huku dakika kutoka nje ya nchi ikiwa bilioni 37.3 na kuwa matumizi ya intanetiyamekifikia 617 PB.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Imelda Banali, alisema serikali kupitia Mfuko wa Mawasaliano kwa Wote (UCSAF), imeanza kupeleka huduma ya mawasiliano maeneo ya mipakani nchini.
Imelda, alisema hatua hiyo itatatua changamoto ya mwingiliano wa mawasiliano baina ya wakazi wa maeneo hayo na wengine nchi jirani kwa lengo la kuboresha huduma hiyo na kuchochea maendeleo katika jamii.
Hata hivyo, alisema Serikali imeweka jitihada kupitia UCSAF kuhakikisha maeneo yote ya mpakani yanafikiwa na huduma hiyo ili kuboresha usikivu wa simu, redio na kuimarisha ulinzi na usalama nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED