Serikali sasa kuifumua reli ya Tazara

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 11:27 AM Jan 10 2025
news
Picha: Mtandao
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akishuka kwenye treni.

SERIKALI iko katika mchakato wa kuifumua na kuiboresha upya reli Tanzania na Zambia (Tazara) ili ifanye kazi kwa ufanisi na kutimiza malengo yake.

Jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alisema hayo baada ya kufanya ziara katika makao makuu ya reli hiyo yaliyoko Tazara.

Alisema ziara hiyo ni maelekezo ya Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa aliyemtuma kwenda kuangalia ufanisi wake na changamoto zilizopo ili serikali izifanyie kazi kwa haraka.

"Nimesafiri na treni ya Mwakyembe kutoka hapa Tazara mpaka Mwakanga ambapo kuna umbali wa Km 20 kwa lengo la kuangalia utendaji kazi wa treni hiyo," alisema Kihenzile muda mfupi baada ya kushuka katika treni hiyo.

Alisema kuwa katika safari hiyo amebaini watanzania wana imani kubwa na usafiri huo na kwamba katika ripoti ya miaka mitatu iliyopita, abiria walisosafiri wamefika zaidi ya milioni tano inayozidi wale wanaosafiri kwenda Zambia, Kidatu mpaka Makambako.  

Kihenzile alisema kuwa kutokana hali hiyo, uwezekzaji wa mabehewa, vichwa vya treni na njia unahitajika lakini tayari serikali ilishayaona hayo na imeanza kuyafanyia kazi.

"Na nimewapa uhakika abiria wetu mnafahamu Rais Samia Suluhu Hassan, miaka miwili iliyopita alifanya ziara Zambia akakutana na Rais wa huko na mwaka jana Septemba marais watatu kutoka China, Tanzania na Zambia walikaa kikao wakakubaliana kwamba lazima reli hii ya tangu mwaka 1975 ifanyiwe maboresho mapya," alisema Kihenzile aliyekuwa ameambatana na baadhi ya maofisa kutoka wizarani.

Alisema reli hiyo ni kongwe na imeharibika sana. Ilikuwa imetengenezwa kubeba mzigo wa tani 5,000,000 lakini ukisoma taarifa ya mwaka jana imefika 447,000 ambayo karibu asilimia tisa ya uwezo wake.

Alisema ukarabarti huo unahitaji muda wa kutosha ili waje na kitu kizuri, akisisitiza lengo lao ni kuwafurahisha wananchi wanaotumia usafiri huo.

Mbali na maeneo ya kufanyiwa ukarabati aliyoyataja Kihenzile, Meneja Mkuu wa Tazara Tanzania, Fuad Abdallah alibainisha maeneo mengine yanayotakiwa kupewa kipaumbele ni uboreshaji madaraja, mahandaki, maeneo ya kubadilishia njia, injini na mabehewa yenye uwezo wa kubeba mzigo mwingi na mzito.

"Sasa tuna changamoto mabehewa ya zamani hayana uwezo wa kubeba kontena nzito, uwezo wa njia ni tani 5,000,000 lakini uwezo wa injini na mabehewa yaliyopo ni tani 500,000," alisema Abdallah