Jahazi lanaswa likisafirisha dawa za kulevya

By Zanura Mollel , Nipashe
Published at 11:05 AM Jan 10 2025
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo.

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata jahazi namba B.F.D 16548 lenye usajili wa Pakistan katika Bahari ya Hindi likisafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo, Aretas Lyimo, alisema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya ukamataji na udhibiti wa dawa za kulevya kwa mwaka 2024 huku akibainisha kuwa jahazi hilo limefanya kazi hiyo kwa miaka 28.

Alisema jahazi hilo limekuwa likifanya safari zake kutokea Pakistan kupitia Iran kwa lengo la kupakia dawa hizo kisha kusambaza nchi mbalimbali za Afrika, ikiwamo Tanzania. 

Mbali na jahazi hilo, alisema raia wanane wa Pakistan walikamatwa na kufikishwa mahakamani jana.

Kamishna Lyimo alisema dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphetamine husafirishwa kwa njia ya jahazi hilo lenye uwezo wa tani nane kwa wakati mmoja.

”Taratibu za kisheria zinaendelea ili pale mahakama itakapojiridhisha, jahazi hilo litataifishwa na kuwa mali ya serikali,” alisema Lyimo. 

Alisema mwaka 2024, mamlaka ilikamata kilogramu 2,327,983,66 za dawa ya kulevya kulinganisha na mwaka 2023 wakati kilogramu milioni 1.9 zilikamatwa na kwamba kiasi hicho ni kikubwa kuwahi kukamatwa nchini. Alisema dawa hizo zingepenyezwa na kuingia sokoni zingekuwa na athari kubwa kwa taifa.

Lyimo alisema bangi ni dawa ya kulevya iliyoongoza kukamatwa kwa mwaka 2024  ikifuatiwa na methamphetamine, heroin na dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya fentanyl. Pia alisema mara ya kwanza dawa mpya aina ya 3-4 Methylne-Dioxy-Pryovalerone(DMV), ilikamatwa nchini.

“Operesheni iliyofanyika mwishoni mwa mwaka ilihusisha ukamataji wa jahazi. Tulikamata kilogramu 673.2 za methamphetamine na heroin na kati ya dawa hizo kilogramu 448.3 ziliwahusisha raia wanane wa Pakistan katika Bahari ya Hindi zikiwa zimefichwa ndani ya jahazi na kilogramu 224.9 zilikamatwa katika fukwe za Bahari ya Hindi mkoani Dar es Salaam,” alisema Kamishna Lyimo.

Katika kuongeza mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Lyimo alisema serikali imenunua boti ya doria inayotarajiwa kuanza kufanya kazi pale taratibu zingine zitakapokamilika ikiwemo uandaaji wa kikosi maalum kwa ajili ya kukabiliana na matukio ya  uhalifu katika Ziwa Victoria, ikiwamo usafirishaji wa dawa za kulevya.

Alisema katika mwambao wa bahari na maziwa kuna zaidi ya vipenyo 600, hivyo mamlaka imejikita kushiririkiana na mamlaka zingine za kiusalama katika kukabiliana na uhalifu. Pia alisema wananchi wamekuwa sehemu kubwa ya kutoa taarifa wanapobaini uwapo wa uhalifu katika maeneo hayo.

Kamishna Lyimo alisema, asilimia kubwa ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya wamekamatwa lakini wako waliokimbilia nchi za nje huku wakiendelea na biashara hiyo.