MWENYEKITI wa Ngome ya Vijana Taifa ACT-Wazalendo, Abdul Nondo, ametoa mapendekezo matano yatakayosaidia kukomesha matukio ya utekaji nchini, akitaka askari polisi kuvaa sare na kujitambulisha wanapokamata raia.
Vilevile, amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan aunde Tume ya Kijaji kuchunguza matukio yote ya mauaji, utekaji na utowekaji raia yaliyotokea mwaka jana ili kubaini watendaji wa uhalifu huo na kuwachukulia hatua za kisheria.
Amesema hayo ukiwa umepita mwezi mmoja tangu alipotekwa na watu wasiojulikana Desemba Mosi mwaka jana saa 10 alfajiri katika Kituo cha Mabasi Magufuli kilichoko Mbezi Luis, Dar es Salaam.
Katika waraka wake aliotoa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari jana, Nondo alisema watanzania wanaweza kutokomeza utekaji na mauji kama wataendelea kuonesha kuchukizwa nayo na kuyapinga.
"Mwaka 2025 uwe mwaka wa kudai uwajibikaji juu ya usalama wa wananchi dhidi ya matukio ya utekaji. Watanzania wote bila kujali itikadi ya vyama vyetu tuungane kwa pamoja kufanya tafakuri, tuhoji na tutake uwajibikaji kwa mamlaka na vyombo husika juu ya usalama wetu dhidi ya matukio ya utekaji na mauaji ambayo yalishika kasi mfululizo mwaka 2024 pasi na majibu ya uchunguzi," alisema.
Kuhusu tume ya kijaji, alisema itatoa majibu ya uhakika kwa kuwa miongoni mwa watuhumiwa wa utekaji na mauaji ya raia ni askari polisi.
"Tume huru ya kijaji kuchunguza itasaidia kujua wahusika na kuwawajibisha na itapunguza wimbi la matukio ya utekaji nchini. Tupaze sauti zetu kutaka Jeshi la Polisi kufuata sheria na taratibu wakati wa ukamataji kwa kuvaa sare, kujitambulisha na kueleza sababu za kukamata mtuhumiwa.
"Hii itasaidia jamii na mkamatwaji kutofautisha ukamataji wa Jeshi la Polisi na watekaji wanaojitambulisha ni Jeshi la Polisi bila kuvaa sare wala kuonesha vitambulisho," alifafanua.
Nondo alisema polisi wasipofuata utaratibu huo, hakutakuwa na tofauti kati ya wahalifu wa utekaji na vyombo vya ulinzi na usalama.
"Ni lazima mstari wa utofauti uchorwe ili kuongeza imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi," alisema.
Nondo alipendekeza pia kuwa ni wakati wa watanzania kupaza sauti ili Jeshi la Polisi libakie kuwa chombo pekee cha ukamataji wahalifu nchini.
Nondo alisema ili kuipa polisi nguvu, Sheria ya Usalama wa Taifa kifungu cha 4(3) kinachoruhusu Ofisa Usalama wa Taifa kukamata mwananchi bila kutoa maelezo ya kosa wala anakompeleka, kinapaswa kufutwa.
Alisema kifungu hicho kimeongeza mwanya wa matukio ya utekaji nchini, akifafanua: "Inawezekana kabisa kifungu cha sheria hii kilikuwa na nia njema ila kwa sasa kinatumika vibaya au kuna kikundi cha watu kinatumia mwanya wa sheria hii kwa maslahi binafsi.
"Ni muda sasa watanzania tuungane kuitaka serikali na Bunge kufuta kifungu hiki ili mamlaka ya ukamataji yabaki chini ya Jeshi la Polisi tu. Hii itafanya Jeshi la Polisi kuwajibika kikamilifu na pia kuondoa mwanya wa watu au kikundi cha watu wanaotumia sheria hii vibaya," alishauri.
Nondo alisema njia nyingine itakayokomesha utekaji na mauaji ya raia ni chombo huru cha kiraia cha kupokea malalamiko ya wananchi dhidi ya matendo ya Jeshi la Polisi, ambacho pia kitachunguza mwenendo wa utendaji wa jeshi hilo.
"Chombo hiki kitasaidia kuwajibisha Jeshi la Polisi, kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria, taratibu, taaluma, haki na kulinda utu," alisema Nondo.
Kuhusu kutekwa kwake, alisema waliomteka walimwonya asiseme kilichomkuta wala kuendelea kuandika mitandaoni na kwamba akifanya hivyo watamteka na kumuua.
Alisema tukio hilo lilihatarisha maisha yake kiasi cha kusababisha figo yake moja kufeli kukaribia kushindwa kazi.
"Figo yangu ambayo ilikuwa inakwenda kufeli (Renal Failure) inaimarika na kufanya kazi, majeraha ya mwili, miguu na mikono kuendelea kuimarika sasa ninaendelea na matibabu nikiwa nyumbani na ninaimarika kiafya kwa uwezo wa Mungu," alisema Nondo.
Alisema ameshakiuka masharti aliyopewa na watekaji kwa kuwa hawezi kuacha kuwatetea vijana na kutoa maoni na mawazo kwa ustawi na maslahi ya jamii na Tanzania.
"Ikiwa wataniteka tena na kuniua kwa kuvunja masharti yao kama walivyoahidi, basi na iwe hivyo ili maandiko ya Mungu yatimie ya kwamba kila nafsi itaonja umauti. Utofauti wa mawazo, itikadi au fikra havipaswi kuwa tiketi ya kuteka au kuua mtu yeyote," alisema.
Nondo alisema upande usiopendezwa na maoni au mawazo mbadala, unapaswa kufuata sheria na mifumo ya haki kumshughulikia mtu anayeonekana kutenda uhalifu na si kumteka.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED