Mradi bomba la mafuta ECOP wafikia asilimia 30- Mramba

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 02:13 PM Jul 10 2024
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda ya TPDC kwenye maonesho ya sabasaba yanayoendelea barabara ya Kilwa Temeke Dar es Salaam
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda ya TPDC kwenye maonesho ya sabasaba yanayoendelea barabara ya Kilwa Temeke Dar es Salaam

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba amesema mradi bomba la mafuta la ECOP kutoka Ohima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga unaendelea na umefikia asilimia 30.

Mramba ameyamebainisha hayo katika banda la Shirika la Maendeleo Petroli Tanzania(TPDC)  alipotembelea katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa  maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es salaam.

"Mradi huu wa mafuta ghafi mpaka mwakani mwishoni mradi utakuwa umekamilika kulingana na ratiba ya mradi na hivi ninavyozungumza tayari kilomita zaidi ya 600 za mabomba zimetandikwa chini mambo yanaenda vizuri ila kwa sababu mabomba yapo chini hayaonekani yamefikiwa,"amesema Mhandisi Mramba. 

Amesema mpaka sasa mradi huo umeshafanyiwa usanifu,ulipaji fidia ambapo wamebaki watu wachache ambao wana mambo ya mirathi.

Katika hatua nyingine Mramba amesema Serikali inatarajia kuongeza vituo vya kujaza gesi asilia kwenye magari kutoka viwili  hadi vituo zaidi ya  30 vilivyopo mkoani Dar es Salaam.

Amesema  ifikapo  mwaka 2025 vituo hivyo vitawawezesha wananchi  kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.

"Mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu tutakuwa tumejenga vituo maeneo ya Muhimbili,Kibaha,Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM),Sinza ,Mwenge,Goba ,Mbezi Beach na Mbagala,‘amesema Mramba.

Amesema kulingana na utaratibu  uliopo vituo hivyo vya kujaza gesi kwenye magari  baadhi vitajengwa na TPDC huku vingine vikitarajiwa kujengwa na sekta binafsi.

Pia amesema TPDC imejiongeza pamoja na kujenga vituo  kwa mfumo wa kawaida uliozoeleka pia wataleta magari ambayo yatauza gesi huku yanatembea.

Aidha amesema mpaka mwakani  kutakuwa na magari mengi  yanaegesha huku akitolea mfano kuwa siku fulani wakiamua kuegesha Mwananyamala itakaa hapo na wateja wa maeneo hayo wataendana magari yao ili wajaziwe gesi.

Aidha alitoa wito kwa TPDC kuhakikisha wanatanua wigo wa usambazaji wa gesi asilia kwa kushirikiana na sekta binafsi. Lengo ni kuhakikisha gesi asilia inawafikia Watanzania wengi zaidi kwa haraka.