Maktaba Jumuishi Kitaifa kuzinduliwa hivi karibuni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:56 AM Jan 14 2025
Mkurugenzi Mkuu wa (TLSB), Dk. Mboni Ruzegea.
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mkuu wa (TLSB), Dk. Mboni Ruzegea.

BODI ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), inatarajia kuzindua maktaba jumuishi ya kitaifa hivi karibuni.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa (TLSB), Dk. Mboni Ruzegea, wakati akizungumzia mkutano wa waandishi na wachapishaji wa vitabu kuhusu Sheria ya amana kwenye maktaba mtandao wa taifa na ununuzi wa vitabu kwa ukuzaji wa soko la ndani utakaofanyika kesho Jumatano.

Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya  Wakurugenzi  ya (TLSB), Profesa Rwekaza Mukandara.

Alisema kuwa mkutano huo utafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa TLSB Maktaba Kuu ya Taifa na kwamba lengo ni kujadili kwa pamoja utekelezaji wa sheria ya amana katika mfumo wa maktaba mtandao wa taifa na ununuzi wa vitabu kutoka kwa waandishi na wachapishaji wa ndani.

Alisema TLSB iliyoanzishwa kwa Sheria ya mwaka 1975 inawapa mamlaka ya kuendeleza masuala ya maktaba kwa kuhakikisha nchi inakuwa na vitabu vya kutosha kupitia maktaba.

“Mkutano huu  wa kesho unalenga tunachofanya kila siku kwa hiyo tunataka kuzungumza na wachapishaji na wazalishaji  kuhusu ubora wa wanachozalisha ili kiweze kuingia kwenye maktaba zetu,” alisema

 Alisema mchapishaji au mwandishi binafsi, kampuni au taasisi kisheria lazima awasilishe nakala ya kitabu chake maktaba kuu ya taifa ili kiwekwe kama urithi kwa kizazi kijacho.

Alisema kumekuwa na mapinduzi ya kiteknolojia kwenye maktaba na  bodi ina mfumo wa maktaba jumuishi ya kitaifa itakayozinduliwa hivi karibuni ambapo TLSB  itakuwa na uwezo mkubwa wa kubadilishana taarifa rasilimali na mtandao wa maktaba zetu.

Tuko mikoa 22 na maktaba zote ziko 43 na bado tuna maktaba jamiii tunamtandao mkubwa na unaendelea kutanuka na maktaba mtandao itarahisisha wananchi wengi kupata huduma zetu,”

“Zamani mtu alikuja na vitabu vinapokelewa vinasajiliwa lakini sasa vinaletwa kwa mtandao, wachapishaji wote wataleta kwa mtandao kwa hiyo itawawezesha wananchi wengi wanapata huduma za maktaba popote walipo,” alisema

“Vitabu vyao vitajulikana na kusomwa kmataifa na hiyo haimaanishi kuwa haki zao za miliki zitakiukwa hapana. Haki zao za umiliki zitazingatiwa haziwezi kupotea kwasababu kuna mfumo wa kulinda haki za wabunifu,” alisema