CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kimeanza kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike katika shule mbalimbali za sekondari jijini Dar es Salaam na wanawake namna ya kutumia digitali na uvumbuzi katika masuala ya afya.
Wameamua kuyajengea uwezo makundi hayo baada ya kuona idadi ndogo ya ushiriki katika matumizi ya teknolojia na uvumbuzi katika sekta ya afya.
Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Emmanuel Balandya, jana katika kongamano la nne la wiki katika masuala ya digitali kwenye sekta ya afya, lililofanyika chuoni hapo, amesema utafiti waliofanya wamebaini ushiriki mdogo wa wanawake na mabinti katika matumizi ya teknolojia.
Prof. Balandya, amesema kongamano hilo limeanza mwaka 2021 na kwa sasa ni mara ya nne kufanyika na linasaidia kuboresha mifumo ya digitali kusomana katika kila sekta.
“ Tumeona kuwa kidogo cha matumizi ya digitali katika sekta ya afya na ili tunafanikiwe na kufika mbali lazima tuanze kuwatengeneza wataalam kuanzia chini na hapa ni watoto wetu hususani wa kike ambao ushiriki wao katika masomo ya sayansi ni mdogo, kupitia mkakati huu tuwasaidia kuongeza idadi na kulisaidia taifa kuwa na wataalam wataosaidia mifumo hiyo,” amesema Prof. Balandya.
Ameongeza kuwa MUHAS wanataka mifumo yote ya kisekta isomane, ili kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na Afya.
“Katika sekta ya afya bado hatufanyi vizuri katika suala la utunzaji na utoaji wa taarifa aidha za wagonjwa na kumbukumbu nyingine, tunahitaji kushughulikia suala hili, kusaidia utunzaji wa taarifa kidigitali badala ya kuhifadhiwa kwenye vitabu,”ameongeza Prof. Balandya.
Amesema wataendelea kuzalisha wataalam kwa ajili ya kusaidia kuingiza mifumo yote inayotoa huduma za kijamii kusomana kigitali kwa kuzingatia miongozo ya Serikali.
Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Ufundi, Idara ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk. Mwajuma Lingwanda, amesema ushiriki wa mabinti na wanawake kwenye matumizi ya kidigitali itaziba pengo lililopo la idadi yao ndogo ya ushiriki.
Dk. Mwajuma amesema kama lengo la kongamano hilo linavyojieleza kuziba pengo na uunganisha wanawake na mabinti katika matumizi ya digitali.
“Hakuna mtu anayepaswa kuachwa nyuma katika mabadiliko kidigitali tunayoyapitia, wanawake na wasichana tunawategemea sana kwa sababu ndio idadi kubwa kwa hiyo lazima washiriki lakini hili ni suala pana zaidi, si suala la teknolojia pekee linahusu pia usawa, uwezeshaji, na maendeleo ya binadamu,” amesema Dk. Mwajuma.
Ameongeza, “wakati tunapojikita katika kuunganisha wanawake na mabinti katika mustakabali wa kidijitali, kuna changamoto muhimu ambazo tunahitaji kushughulikia ikiwemo vizuwizi wanavyokutana navyo wanawake katika kupata teknolojia taarifa za kidigitali katika masuala ya afya”.
Amesema kushinda vizuwizi hivyo ni muhimu kusikiliza sauti za wanawake na mabinti na kuelewa changamoto zao maalum na fursa zilizopo, watafiti wa MUHAS, mtusaidie kushughulikia ili kusaidia wanawake na mabinti kung'ara katika mageuzi ya sekta ya afya kidijitali.
Ameongeza kuwa Wizara, imedhamiria kutekeleza maono hayo, tutaendelea kukuza elimu ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, na Hisabati (STEM) kwa wasichana, kuongeza upatikanaji wa rasilimali za kidijitali na kujenga majukwaa yatakayohamasisha ubunifu na uongozi miongoni mwa wanawake.
Amedai wamejidhatiti kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya mabadiliko ya kidijitali na yatakuwa kichocheo cha usawa wa kijinsia na maendeleo ya kiuchumi nchini.
Debora Enock, mwanafunzi wa shule ya sekondari Mbezi Inn, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwao kwani yatawasidia kujua ni kwa namna gani wataitumia digitali kupata taarifa katika sekta ya afya.
Kalyne Mseki, mwanafunzi wa kidato cha sita shule ya sekondari Jangwani, amesema katika kuhakikisha kuna idadi kubwa ya wasichana na katika matumizi ya digitali ni muhimu Serikali kwa kushirikiana na wadau wakawekeza kwenye ununuzi wa vifaa shuleni.
Amesema hatua itasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kujua namna masuala ya teknolojia yanafanya kazi na kuwahamasisha kutumia maarifa hayo hata wanapohitimu shule.
“ Tunafurahi kuwa sehemu ya kongamano hili, ni kweli kuwa idadi yetu wasichana katika matumizi ya teknolojia ni ndogo lakini mpango huu utatuhamasisha lakini ili kufikia malengo hayo lazima uwekezaji katika vifaa ufanyike kwa kuzingatia pia watu wenye ulemavu, shule ziwe na teknolojia kwa ajili ya kujifunza,” amesema Kalyne.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED